Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 


Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake - 3
 
Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili
Imekusanywa Na: Abu Faatwimah 

Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake - 3


Katazo La Kujizuilia Kulala [Kustarehe] Na Mume Anapomuhitaji
Huu dada yangu katika iymaan ni uwanja wenye hatari kubwa, na wengi miongoni mwa wanawake kwa visingizio visivyokuwa na misingi wameuingia na kugaragara ndani yake; hivyo imewawajibikia kwa hilo laana ya Malaika wa ar-Rahmaan kwa kuwa waume zao hawakuridhika nao bali walighadhibika nao.


Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mume atakapomwita mkewe kwenye kitanda chake [kwa tendo la ndoa] na yule mke akakataa kumuitika, Malaika humlaani mpaka kupambazuke” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Nikaah, mlango wa atakapolala mwanamke hali ya kuwa amekihama kitanda cha mumewe. Hadiyth namba 4821 na namba 4822; Muslim, kitabu cha Nikaah, mlango uharamu wa mwanamke kujizuilia [kujitenga] na kitanda cha mumewe, Hadiyth namba 2602 na Hadiyth namba 2603 na 2604.]
Hadiyth hii na nyengine kama hii dada yangu katika iymaan inabainisha na kuthibitisha kuwa mume ana haki kwa mkewe kama alivyo na haki mke kwa mumewe; na miongoni mwa hizo haki ni hii haki ya kustarehe na mkewe, na ni haramu kwa mke kujizuilia kutekeleza haki za mumewe ikiwemo hii haki ya kustarehe nae; hivyo wakati wowote ule mke akijizuilia kustarehe na mumewe hujiwajibishia laana ya Malaika [dua ya kumuombea maangamizo ya ku*****uzwa kutoka kwenye Rahmah ya Allaah].
Vipi utakuwa ikiwa Malaika wa ar-Rahmaan watakuapiza? Vipi itakuwa hali yako wakati umesimama mbele ya Jabbaar Siku ya Qiyaamah, unahesabiwa amali zako na katika amali zako mbovu na chafu imo hii ya kujizuilia kustarehe na mumeo?
Mke huruhusika kujizuilia kustarehe na mumewe kama atakuwa mgonjwa au ana udhuru wenye kukubalika kishari’ah, kama vile yuko katika siku zake au amefunga Swawm ya waajib, na humuwajibikia kumuitika mumewe kama atamuhitaji wakati wowote ule utakapotoweka udhuru.

Katazo La Kufunga Sawm Ya Sunnah Bila Idhini Ya Mume
Wanawake wengi huwa wanapendelea kufunga Swawm za Sunnah; na wakati mwingine kwa pupa zao za upendaji wao wa mambo ya kheri na kutaka kujikumbia fadhila zilizofungamana na Swawm za Sunnah utawaona wanakimbilia kutekeleza Swawm za Sunnah au hata kutaka kuzitanguliza kabla ya kutimiza za waajib; wakisahau kuwa Swawm ya wajibu [fardhi] ni deni na isipotekelezwa huwa ni kosa kinyume na utekelezaji wa Swawm ya Sunnah ambayo ni jambo la mtu kujipendekeza kwa Muumba wake.  
Kwa hali hii huwapelekea wengi miongoni mwa dada zangu katika iymaan kujifungia Swawm ya Sunnah kwa kutafuta fadhila na kujikurubisha kwa Allaah bila ya kuelewa kuwa huyo wanayetaka kujikurubisha Kwake na kwa kuwapatia Fadhila Zake, Amewataka kwa kupitia Mjumbe Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wawe na hadhari ya kutofunga Swawm yoyote ile ya Sunnah bila idhini ya waume zao.
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asifunge mwanamke [Swawm ya Sunnah] na huku mumewe yuko pamoja nae isipokuwa kwa idhini yake huyo mume na wala asimruhusu mtu katika nyumba ikiwa mumewe yuko isipokuwa kwa idhini yake huyo mume” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Nikaah, mlango wa Swamw ya Sunnah ya mwanamke kwa idhini ya mumewe, Hadiyth namba 4820; na katika Kitabu cha Tafsiri Qur aan, Suuratul Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 4823; na Muslim, katika Kitabu cha Zakaah, mlango wa atachotoa mtumishi katika mali ya tajiri wake, Hadiyth namba 1710].
Imaam An-Nawawiy amesema: Hii inakusudiwa Swawm ya Sunnah na Swawm zote zisizokuwa za nyakati maalumu, na hili katazo la uharamu liko wazi, na sababu yake ni kuwa mume ana haki ya kustarehe na mkewe katika siku zote za wiki, na haki hii ni waajib ulio wa haraka; hivyo haiwezi ikaondoka [ikaporomoka] au kudondoshwa kwa Sunnah wala kwa jambo la waajib lisilo la haraka.
Na kauli yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “... na huku mumewe yuko pamoja nae na maana kama kama mume atakuwa safarini na mke yuko nyumbani, mke huyo atakuwa huru kufunga Swawm ya Sunnah.
Katazo La Kutoa Chochote Kutoka Katika Nyumba Bila Idhini Yake Mume
Katika desturi na kawaida za watu kutoa walichonacho kinapohitajiwa, na wakati mwingine wahitaji hupita katika nyumba na kuomba wasaidiwe na wahusika wa hizo nyumba huwa wako katika shughuli zao za kawaida za kutafuta riziki za halali, hivyo hukutana na wachunga wa hizo nyumba ambao huwafungulia milango na kusikiliza maombi yao; kama haja ya dharura basi huwa hawana budi isipokuwa kuitafutia ufumbuzi kama uko ndani ya nyumba; na kama haja si ya dharura basi si vyema kwa mke kufungua mlango na kujiingiza katika mazungumzo na wasio kuwa Mahaarimu zake; na itapobidi kutoa basi atowe bila ufisadi na atowe kwa ajili ya Allaah na sio kumpatia amtakae kwa sababu duni za kidunia.
Mke ni vyema aelewe kuwa yeyé ni msimamizi na mchungaji katika nyumba ya mumewe na kuwa atakuja kuulizwa kuhusu usimamizi na uchungaji huo. 


Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ee!! Jueni ya kwamba nyie nyote ni wachunga na kila mmoja ataulizwa alichokichunga, kiongozi wa watu ni mchunga na ataulizwa kwa alichokichunga, na mwanamme ni mchunga wa familia wake na ataulizwa kwa alichokichunga, mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mume wake na watoto wake naye ataulizwa alichokichunga, na mtumwa ni mchunga wa mali ya bwana wake naye ataulizwa kuhusu uchungaji wake” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Hajj, milango ya Al-Muhswar na Jaza ya kiwindo, Hadiyth namba 2381 na 2384 na 2560; na katika Kitabu cha Tafsiri Qur-aan, Suuratul Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 4816 na 4828; na Muslim, katika Kitabu Al-Imaarah, mlango wa fadhila za Al-Imaamu Al-‘Aadil [Muadilifu]……, Hadiyth namba 4314].
Dada yangu katika iymaan fahamu na uelewe kuwa nyumbani kwako kuna majukumu mengi na makubwa mno, kwa hivyo yahifadhi vizuri kwa kuyatekeleza kama ipasavo; ihifadhi mali ya mume wako na katika hiyo mali ni nyumba na kila kilichomo ndani yake.

Hifadhi nzuri ya mali ya mume huwa ni katika mipango mizuri ya kuchunga nyumba kwani huwa iko mbali na ubadhirifu au israfu, pia kutotoa kitu chochote kile hata kiwe kidogo vipi kutoka katika nyumba bila ya idhini ya mume ni katika kuchunga mali ya mume. 


Imepokelewa kutoka kwa Abu Umaamah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asitoe mwanamke kitu chochote kutoka katika nyumba ya mumewe isipokuwa kwa idhini ya mumewe.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Nikaah, mlango wa Swawm ya Sunnah ya mwanamke kwa idhini ya mumewe, Hadiyth namba 4823; na Muslim, katika Kitabu cha Zakaah, mlango wa atachotoa mtumishi katika mali ya tajiri wake, Hadiyth namba 1710].
Hadiyth hii inatuongoza na kutubainishai kuwa inampasa mke kupata idhini ya mumewe katika kutoa kitu chochote kile katika mali ya mumewe; na makusudio ya kutoa hapa ni: kutoa mali katika njia za kisharia kama kutoa Zakaah au Swadaqah au kumsaidia mpita njia au aliye haribikiwa na kukatikiwa na msaada.
Mke atakapotoa katika njia hizi za kishari’ah kutoka katika mali ya mumewe kwa shuruti ya kuwepo idhini ya huyo mume [iwe kwa kumtaka idhini au awe amepewa idhini kabla kama ikitokea kuhitajika kutoa basi nimekuruhusu kutoa kiasi kadha na katika jambo kadha] hupata thawabu za kutoa na mume hupata thawabu za uchumaji wa hiyo mali iliyotolewa.
Kutoka kwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakapotoa mwanamke kutoka katika chakula cha nyumba yake huyo mwanamke (na katika riwayah: katika nyumba ya mumewe) bila ya kufisidi [uharibifu], atapata ujira wake kwa kile alichotoa, na mumewe atapata ujira wake kwa kile alichochuma...” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Ijumaa, milango ya ‘amali katika Swalah, Hadiyth namba 1353, 1355 na 1356; na kitabu cha Hajj, milango ya Al-Muhswar na Jaza ya kiwindo, Hadiyth namba 1934; na Muslim, katika Kitabu cha Zakaah, mlango wa ujira wa Mhifadhi [khaazin] mwaminifu na mwanamke atakapotoa..., Hadiyth namba 1706 na 1707].
Hadiyth imebainisha kuwa wote wawili watapata thawabu [mke kwa kutoa  na mume kwa sababu ya mali iliyotolewa ambayo aliichuma]; ni uzuri ulioje kwa mume aliyekarimu kwa mali yake na mke aliyemwepesi kutoa kutoka katika mali ya mumewe bila ya uharibifi na utoaji wenyewe katika Njia ya Allaah.
Katazo La Kumuasi Mume


Mke kumuasi au kumdharau mumewe ni katika madhambi makubwa; mke anatakiwa awe mnyenyekevu mbele ya mumewe, asimwangalie mumewe kwa jicho la ufedhuli, asimnunue wala asimgomee, amtii anapomwamrisha, anyamaze na kumsikiliza anapomsemesha, amsikilize anapozungumza, amkaribishe anapoingia nyumbani, amuage anapoondoka nyumbani, ampokee anapokuja na kitu, ajiepushe na mambo yanayoweza kumkasirisha au kumuudhi, aridhike na kidogo chochote anacholetewa, asimkalifishe kwa asiyoyaweza.
Allaah Anasema: “… Basi Swaalihaatu [wanawake wema] ni Qaanitaatu [wale wenye kutii] na ni Haafidhaatu [wanaohifadhi heshima zao na mali za waume zao] hata katika siri [wanapokuwa hawapo] kwa Aliyoyahifadhi Allaah [Aliyoyaamrisha Allaah kuhifadhiwa]. Na wale [wanawake] ambao mnachelea uasi wao, basi wapeni mawaidha [wanasihini], [wakiendelea na uasi, basi] muwahame katika malazi na muwapige. [Watakapo rejea katika twaa’ah] msiwatafutie njia ya kuwaudhi bure…” [An-Nisaa 4: 34].
Ni juu ya mwanamke swaalihah kumtendea wema mumewe na kukaa nae kwa ihsaan; kumsikiliza kama itakiwavo na kumtii katika mambo yasiyo ya maasi, kwani hakuna utiifu kwa kiumbe yeyote yule katika maasi; mke atakapoamrishwa na mumewe katika yenye kumghadhibisha Mola na katika yenye kwenda kinyume na maamrisho au mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huwa hatakiwi kutii wala kusikiliza katika hilo.
Kutoka kwa Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kumwambia yeye Ibn Mas’uud (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Utakuwa na hali gani ee ‘Abdullaah! Mtakapokuwa na viongozi wenye kupuuza [kutojali] Sunnah na kuchelewesha Swalah na nyakati zake? Akasema: Nini unaniamrishwa ewe Mjumbe wa Allaahu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)! Akasema: Unaniuliza cha kufanya Ibn Umm ‘Abdi?! Hakuna kutii [amri yoyote yule ya] kiumbe katika yenye kumuasi Allaah…” [Imepokelewa na Ahmad, kitabu Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad Mukthiriyna katika Swahabah (Radhiya Allahu ‘anhum), Hadiyth ya Ibn Mas’uud (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 3757 na kitabu Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Awwalul Musnadul Baswariyyina, Hadiyth ya ‘Imraan bin Huswayn (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 20150].
Amesema Ibn al-Jawziy: Kuhusu kuwajibika mke kumtii mumewe, ni kuwa haijuzu kwa mke kumtii mume katika yasiyokuwa halali, kama vile atakapo mtaka kumuingilia kwenye duburi [utupu wa nyuma] au kumuingilia wakati akiwa katika hedhi, au katika mchana wa Ramadhaan, au katika yasiyokuwa hayo katika maasi.
Mke hutarajiwa kumtii mumewe katika kila lenye kueleweka kuwa ni ma’aruuf; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewaamrisha wanawake kuwatendea wema waume zao na kukaa nao kwa ihsaan; na kuwasikiliza na pia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewakataza wanawake kuwaasi waume zao na kuwatendea maovu kwa sababu na hekima aijuayo yeye Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hekima iliyompelekea [Allaahu A’alam] kufikia kusema: " …. lau kama ningelikuwa wa kumwamrisha mmoja yeyote amsujudie mmoja; basi ningelimwamrisha mwanamke kumsujudia mumewe, lau mumewe angelimwamrisha kuchukua [kitu] kutoka jabali manjano kupeleka jabalí jeusi na kutoka mlima mweusi kupeleka mlima mweupe, basi ingekuwa juu yake [mke] kutekeleza” [Imepokelewa Ahmad, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Saadis ‘Ashar Al-Answaar, Hadiyth ya mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anhaa), Hadiyth namba 23912; na Ibn Maajah, katika Kitabu cha ndoa, mlango wa haki ya Mume juu ya ya mkewe, Hadiyth namba 1842].
Dada yangu katika iymaan ni hakika isiyokuwa na mjadala kuwa mwenye kumuasi mtu yeyote huwa hakuna njia ya aliyeasiwa kumpenda mtu huyo; hivyo basi utapomuasi mumeo kwa kwenda kinyume na matakwa yake si tu unakwenda kinyume na mafundisho aliyokuja nayo Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa unastahiki anayostahiki kila mwenye kwenda kinyume na amri zake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam); bali pia utakuwa umejitoa katika mapenzi ya huyo mume na kumpelekea kutokuwa na furaha yoyote ile wakati anapokutazama au kuona au hata kusikia sauti yako na huenda ukampelekea kuwa miongoni mwa wanaume wenye wake lakini wakati wao wote wanaupitisha nje ya nyumba zao kwa kutopenda kuwaona wake zao kwa maudhi yao, jambo ambalo huenda likakupelekea kujiondoa katika wenye kueleweka kuwa ni wanawake wazuri na bora miongoni mwa wanawake kama ilivyothibiti.
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba aliulizwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wanawake gani bora? Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Ambae humfurahisha [humpendezesha] anapomtazama, na humtii anapomwamrisha, mke humhifadhi katika nafsi yake na mali ya mumewe” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad waliobakia katika Mukthiriyna katika Swahaabah (Radhiya Allahu ‘anhum), Musnad Abi Hurayrah (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 7245 na 9377 na 9445].
Pia Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah hamtazami mwanamke yeyote yule asiyekuwa na shukurani kwa mumewe, naye hawezi kujitosheleza bila ya huyo mume”  [Imepokelewa katika Mustadrak ya Swahiyhayn, katika Kitabu cha Imaamah na Swalah ya Jama’ah, mlango wa Taamiyn, Hadiyth namba 2696; na katika Kitabu cha kuwajua Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), kutajwa kwa fadhila za makabila, Hadiyth namba 7416 na 7417; na An-Nasaaiy, katika Kitabu cha ‘Ish-ratun Nisaa, milango ya Mulaa’abah, Hadiyth namba 8803 na 8804; na Al-Bayhaqiy katika Kitabu cha Wasiya, Jimaa’u milango ya kuwaendea wanawake, Hadiyth namba 13637].
Ni juu ya kila mwanamke swaalihah kutafuta radhi za Mola wake kupitia radhi za mumewe kwa kumtii mumewe, na kutokwenda kinyume na amri zake kwa kumfanyia ujeuri, ufedhuli au usafihi au maovu yoyote yale, yawe ya kauli au vitendo; kwani mume huenda ikawa Jannah ya huyo mke au huenda ikawa Moto wake; kutoka kwa ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:“Atakaposwali mwanamke Swalah zake tano; na akafunga mwezi wake [Ramadhaan]; na akahifadhi sehemu zake za siri; na akamtii mume wake; ataambiwa [Siku ya Qiyaamah]: Ingia Jannah kupitia mlango wowote uutakao katika milango ya Jannah” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad waliobaki katika kumi waliobashiriwa Jannah, Hadiyth ya ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf (Radhiya Allahu ‘anhu), Hadiyth namba 1595; na Ibn Hibbaan, katika kitabu cha Ndoa, mlango wa mu’aasharah wanandoa wawili, Hadiyth namba 4252]
Katazo La Kudai Talaka Bila Ya Sababu Inayokubalika


Ndoa ni katika mambo Aliyoyaamrishwa Allaah na kuyahimiza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ndoa ni mafungamano ya kishari’ah baina ya mwanamme na mwanamke yenye mipaka, nidhamu, vidhibiti na kanuni maalumu; na inaathiri mengi; ima kujenga na kusimamisha familia ya Kiislamu yenye kuongozwa na kuongoka kwa uongofu wa Qur-aan na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa miongoni mwa tofali la kuijenga jamii rabbaaniy [yenye kumuabudu Allaah pekee Mola wa viumbe vyote na yenye kufundisha Kitabu, kukisoma na kukifuata]; na ima kuvunja na kubomoa familia kwa kuivuruga vuruga na kuisambaratisha na kusababisha athari mbaya kwa jamii na watoto kwa kuachana kwa mume na mke.
Allaah Alipoweka shari’ah na utaratibu wa ndoa na kuiamrishwa [kwa kuwa Yeye Subhaanah ndie Muumba wetu na ni ‘Aalim wa hali zetu na uwezo wetu, Alielewa kuwa tabia na desturi zetu huenda zisikubaliane, na kwamba mawazo na fikra huenda yasifanane]; hivyo kwa Hikma Yake Akaweka utaratibu wa kuachana na kutengana [talaka] pale panaposhindikana kupatikana njia ya kusuluhisha na kupatanisha baina ya wanandoa wawili.  Hata hivyo Allaah Ameiwekea talaka taratibu, nidhamu na mipaka yake; hatarajiwi kuivuka na kuivunja isipokuwa faasiq; na katika taratibu, nidhamu na mipaka ya talaka ni kuwa haifai kwa mke kumuomba mumewe talaka bila sababu yoyote ile yenye kukubalika kishari’ah.
Hii ni kwa kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke yeyote yule ataemuomba mumewe talaka bila ya sababu yoyote ile, basi ni haramu juu yake harufu ya Jannah“ [Imepokelewa na Ahmad, kitabu Musnad, Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnadul Answaar, Hadiyth namba 21852 na 21789; na Ibn Maajah, katika Kitabu cha Atw-Twalaaq, mlango wa uchukivu wa kujikombowa kwa mwanamke, Hadiyth namba 2044 na 2045; na katika Mustadrak ya Swahiyhayn, katika Kitabu cha Imaamah na Swalah ya Jama’ah, mlango wa Ta-amiyn, Hadiyth namba 2735].
Lau mume atakuwa anamfanyia vitimbi na makruhi [kumpelekea mke kudai talaka] au hampendi lakini anamng’ang’ania na kumtundika kwa kisingizio kuwa anamtia adabu; hili ni kosa kwa upande wa mume. Katika hali hii pia mke hatakiwi kudai talaka yake bali atatakiwa apeleke lalamiko lake kwa Qaadhi au msimamizi wa mambo ya Kiislamu ili ichukuliwe hatua munasibu kwa kumuachisha na mume hatolipwa chochote kwa sababu yeye ndiye mkosa na haitokuwa halali kwa mume kuchukua chochote wala Khul'u haiswihi hapa kama Anavyosema Allaah:
Wala msiwadhikishe ili muwapokonye baadhi ya mlivyowapa - isipokuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Allaah ametia kheri nyingi ndani yake.” [An-Nisaa 4: 19].
Na katika yaliyokatazwa ambayo yameenea na kuzagaa kwa wenye kupenda dunia na kuiweka kando Aakhirah ni kwa mwanamke kumtaka au kumghilibu mumewe; iwe kwa kumhadaa au vinginevyo kwa kumshurutisha amuache mkewe ili apate kuolewa yeye au abakie yeye pekee yake [kama ni mke mwenza] hili limekatazwa kama ilivyothibiti katika Hadiythi kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke asitake (katika Riwayah: Si halali kwa mwanamke kudai kuachwa ukhti wake [mwanamke mwenzake] ili aichukue nafasi yake na kuolewa yeye; kwani hatopata isipokuwa yale aliyoandikiwa.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha tafsiyr ya Qur-aan, Surat Qul A’uwdhu Birabbil Falaq, Hadiyth namba 6141 na 4782; na Muslim, katika Kitabu cha ndoa, mlango wa Uharamu wa kuwakusanya mwanamke na Shangazi yake, Hadiyth namba 2527; na Abu Daawuud, katika Kitabu cha atw-Twalaaq, mlango katika mwanamke anamtaka mumewe talaka ya mke wake, Hadiyth namba1865].


 Posted By Posted juu ya Friday, June 29 @ 17:35:58 PDT na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili:
Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa Rafiki





Mada zinazohusiana

Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili

 

Ẹsin Islam الدين الإسلامي Religion of Islam Addinin Musulunci Agama Islam Religión del Islam 伊斯兰教 Dini ya Kiislamu Религия Ислам Religião do Islã イスラム教 Esin Islam 이슬람의 종교 Portal African Muslim Website - Arabic English African Islamic Website For World News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Articles, Radio, Audio, Video, Quran, Hadith, TV Channels, Fatwas, Muslim News, Newspapers, Magazines Headlines, Forums, College, Schools, Universities, Mosques, Quranic, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Ramadan, Vidoes, Books, Fasting, PDFs On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com