Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 


Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake – 7
 
Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili Imekusanywa Na: Abu Faatwimah

Makatazo Ya Kishari’ah Kwa Wanawake – 7

Katazo La Kujipiga piga Na Kuchana Nguo Wakati Wa Msiba
Msiba ni katika Sunnah na mitihani ya uhai, Allaah Anasema:

“Na bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao. Na wabashirie wenye kusubiri.” [Al-Baqarah 2: 155].

Pia Allaah Anasema:
“Kila nafsi itaonja mauti. Na hakika mtalipwa kikamilifu ujira wenu Siku ya Qiyaamah. Basi atakayewekwa mbali na Moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. Na maisha ya dunia si lolote ila ni starehe ya udanganyifu.” [Aal-‘Imraan 3: 185].



Hii ni kusema kuwa hakuna njia ya kuuepuka kwa kuuchelewesha au kuukadimisha na wala hakuna njia ya kuukimbia; Allaah Anasema:
“Popote mtakapokuwa yataku*****ieni mauti, japo mkiwa katika ngome madhubuti…” [An-Nisaa 4: 78].

Pia Allaah Anasema:
“Sema: “Hakika [hayo] mauti ambayo mnayakimbia, bila ya shaka yatakukuteni…” [Al-Jumu’ah 62: 8]

Dada yangu katika iymaan, msiba ni katika haki na ni miongoni mwa yale yaliyokwisha pitishwa na kukadiriwa na Muumba kuwa utamfikia mwanaadamu kama ulivyopanga na kwa wakati wake maalumu, Allaah Anasema:

“Hautokei msiba katika ardhi na wala katika nafsi zenu isipokuwa umekwishaandikwa katika Kitabu kabla Hatujauumba…” [Al-Hadiyd 57: 22].

Hii ni kusema kuwa msiba hautokei kwa bahati mbaya, wala kwa makosa, na wala hauhitaji sababu, kwani hutokea kwa Elimu na Idhini yake Muumba; Allaah Anasema:

“Na haiwi kwa nafsi yeyote kufa isipokuwa kwa Idhini ya Allaah, imeandikwa muda wake maalumu…” [Aal-‘Imraan 3: 145].

Dada yangu katika iymaan, kuyaelewa na kuyafahamu hayo na kuwa na iymaan thabiti kwayo si jambo jepesi wala si jambo rahisi na wala si jambo la kawaida, ndio Allaah Akaweka ujira mkubwa kabisa kwa kila mwenye kufikiwa na msiba kwa kuupokea kama Atakavyo Yeye kwa kutolalamika na kutonung’unika, bali kuridhika, kusubiri, kushukuru pale ataposema yale aliyoamrishwa na Allaah kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Hakuna Muislamu yeyote yule atakayekumbwa na msiba akasema yale Aliyomuamrisha Allaah: “Innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji’uwn (hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake tutarejea).” [Al Baqarah 2: 156]. "Allaahumma Ajirniy fiy muswiybatiy Wakhluf-liy khayram-minhaa (Ee Allaah Nilipe –thawabu- kwa msiba wangu na nipe -badala yake- bora kuliko huo msiba)- isipokuwa Allaah Atampa badala yake bora kuliko huo msiba…” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa yenye kusemwa wakati wa msiba, Hadiyth namba 1531 na 1532].

Ujira na tunzo anayotunukiwa ni:

“Hao juu yao zitakuwa Barakah kutoka kwa Mola wao na Rahmah, na hao ndio wenye kuongoka.” [Al-Baqarah 2: 157].

Tunzo hii imekusanya mambo matatu: Barakah kutoka kwa Mola, Rahmah na kuwa hao ndio Al-Muh-taduwn (walioongoka), kwa kusubiri kwao kwa msiba uliowashukia.

Dada yangu katika iymaan, ni uzuri ulioje wa fadhila na malipo mema kutoka kwa Muumba Aliyechukuwa kile Alichomtunuku mja akasubiri na akashukuru na akaleta istirjaa’ -innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji’uwn.

Ama wenye kushindwa kusubiri, kushukuru na kuridhia majaaliwa na makadirio ya Allaah na wenye kudhani kuwa kilichochukuliwa ni chao, na kuwa hakikuchukuliwa bali wamepokonywa, huwa na mengi katika yenye kuonyesha na kuthibitisha kuwa si tu hawakuwa tayari, bali kubwa ni kuwa hawakufurahika kamwe, na wala hawakuridhika kamwe kwa msiba uliowasibu, bali huona na kuwa na hisia kuwa wameonewa, wamepokonywa na kunyang’anywa kilicho chao na kudhulimiwa.

Dada yangu katika iymaan, kutokana na mambo kama hayo na mingine mengi ya hayo ndio Waumini wakatakiwa wawe na subira wakati wowote ule wanaposibiwa na msiba si tu wa kuondokewa na vipenzi, kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Amesema Allaah Aliyetukuka: Hana mja Wangu Muumini jazaa Nitakapomchukulia -Mfisha- mpenzi wake katika watu wa dunia, kisha akatarajia thawabu isipokuwa –atapata- Jannah.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Tafsiyr ya Qur-aan, Suurat Qul A’uwdhu bi Rabil Falq, Hadiyth namba 5973].

Na pia katika Hadiyth ya Abu Muusa Al-Ash’ariyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Anapofariki mtoto wa mja –katika Riwaayah ya Ibn Hibbaan: mja Muumin-, Allaah Husema: Ee Malaika wa mauti: Umechukua –katika Riwaayah ya Ibn Hibbaan na At-Tirmidhiyy: Allaah Huwaambia Malaika: Mmechukua- roho ya mwana wa mja Wangu? Umechukua kiburudisho jicho lake? Umechukua tunda la moyo wake! Malaika wa mauti husema: Na’am. Kisha Allaah Husema: Amesema nini mja Wangu? Malaika hujibu kuwa: Amekusifu –kwa kukuhimidi kwa kusema Al-Hamdu LiLLaahi-na amesema kauli ya istirjaa’ -innaa liLLaahi wa innaa ilayhi raaji’uwn-. Allaah Husema: Mjengeeni nyumba katika Jannah na iiteni Baytul-Hamd -nyumba ya shukurani-.” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad wake, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, tatimmat Musnad Al-Kuwfiyyiyna, Hadiyth ya Abu Muusa Al-Ash’ariyy (Radhiya Allaahu ‘anhu), Hadiyth namba 19286; na At-Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Ijumaa, milango ya safari, Hadiyth namba 941, na amesema: Hii ni Hadiyth Hasanun Ghariybun; na Ibn Hibbaan, katika Kitabu cha Al-Janaaiz na yenye kufungamana nayo…, mlango yaliyokuja katika subira na thawabu za magonjwa, Hadiyth namba 3024].

Dada yangu katika iymaan, hayo ni baadhi ya malipo Aliyoyaandaa Mola ambayo hutarajiya kuwafikishwa kuweza kuyapata kila Muumin huko Aakhirah kwa kusubiri kwake; ama hapa duniani kuna ujira mkubwa pia na wenye kuvutia na kupendeza kwa kila Mudh-nibun na Mukh-twiun unapowafikia msiba wa kuondokewa na mpenzi au msiba wa aina nyingine yoyote ile kwa kusamehewa madhambi yao kwa kila kinachowasibu pindi wakisubiri na kutaraji malipo kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Muislamu hafikiwi na tabu wala machovu, wala hamu wala huzuni wala madhara, wala dhiki hata mwiba ukimchoma isipokuwa Allaah Humfutia kwayo makosa yake.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Wagonjwa, mlango wa yaliyokuja katika kaffaar ya ugonjwa…, Hadiyth namba 5238 na 5239; na Muslim, katika Kitabu cha Al-Birr na Asw-Swilah na Aadaab, mlango wa thawabu za Muumini katika yenye kumsibu miongoni mwa magonjwa…, Hadiyth namba 4674].

Dada yangu katika iymaan, ni uzuri ulioje wa fadhila na malipo mema ya Aakhirah na duniani kutoka kwa Muumba Aliyechukua kile Alichomtunuku mja, Mola Aliyeandika mja kufikiwa na tabu, machovu, hamu, huzuni, madhara, dhiki, maradhi, kuchomwa na mwiba na kadhalika, akasubiri, akashukuru na akasema yale aliyomuamrisha Mola wake.

Dada yangu katika iymaan, kinachotakiwa kwa aliyefikwa na msiba ni kusubiri na kwa kila mwenye kwenda kutoa mkono wa pole –ta’ziyah- kusisitiza subira na kuhimiza kuridhika kwa yale Aliyoyapitisha Allaah na kumbashiria malipo makubwa yasiyokuwa na hesabu ya wanaosubiri; Allaah Anasema:

“Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao bila ya hesabu.” [Az-Zumar 39: 10].

Dada yangu katika iymaan, ukweli ni kuwa si kila mwenye kufikwa na msiba huweza kufikia kuingia katika wale wenye kutarajia malipo makubwa na yasiyo na hesabu yaliyoahidiwa na Mola; dada yangu katika iymaan, mimi na wewe tunao mfano mzuri kwa mwanamke katika wenye subira yenye kupelekea kuweza kufikia daraja ya kutodhihirisha hata huzuni wakati wa msiba kama ilivyothibiti kwa Swahaabiyyah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) miongoni mwa Swahaabiyyaat (Radhiya Allaahu ‘anhunna) wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama inavyosimuliwa kuwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisikiwa akisema kuwa:

“Abu Twalhah alifiwa na mtoto aliyezaa na Ummu Sulaym. Ummu Sulaym akawaambia jamaa zake: “Msimweleze Abu Twalhah mpaka mimi niwe ndiye nitakayemweleza” Aliporudi, akampelekea chakula cha jioni, akala na akanywa, kisha –Ummu Sulaym- akajipamba kuliko anavyojipamba siku zote. Abu Twalhah akamjamii. Ummu Sulaym alipoona kuwa Abu Twalhah ameshiba na amemjamii alimwambia: “Ee Abu Twalhah! Niambie lau watu wameazima kitu kwa watu fulani, kisha walioazimwa wakataka kitu chao kilichoazimwa, je, walioazima wana haki ya kuwanyima?” Abu Twalhah akajibu: “Hapana!” Ummu Sulaym akamwambia: “Basi taraji thawabu kwa msiba wa mwanao.” Abu Twalhah akakasirika na akasema: “Umeniacha mpaka nimejichafua [kwa jimai] halafu ndio unaniambia habari ya msiba wa mwanangu?” Abu Twalhah akaenda kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamueleza mambo yalivyokuwa. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaombea kwa kusema: “Allaah Awabarikie katika usiku wenu.” Ummu Sulaym akabeba mimba. Akazaa mvulana. Abu Twalhah akaniambia: “Mbebe umpeleke kwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).” Akapeleka na tende kadhaa. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: Ana kitu? Akajibu: “Ndio, tende kadhaa.” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akazichukua akazitafuna kisha akachukua zile tende zilokuwa mdomoni mwake akazitia katika kinywa cha mtoto, halafu akamsugulia nazo (ili mtoto afyonze na kumeza) na akampa jina la ‘Abdullaah…” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa asiyedhihirisha huzuni zake kwenye msiba, Hadiyth namba 1225; na Muslim, katika Kitabu cha fadhila za Swahaabah (Radhiya Allaahu ‘anhum), mlango wa katika fadhila za Abi Twalhah al Answaariy, Hadiyth namba 4503].

Dada yangu katika iymaan, huo ni mfano mzuri na wa aina yake wa kutodhihirisha huzuni wakati wa msiba wa kipenzi wenye kutaka kuigwa, na kuacha kuiga mifano ya wenye kushindwa kuvuta subira na kujizuia, jambo linalowapeleka kuanza kuwa kama waliopoteza fahamu na kurukwa na akili zao; hivyo utawaona wanajipiga piga, na wakati mwingine wanachana chana nguo zao na kubwa kuliko hayo yote ni huku kufunua midomo yao na kuanza kutoa matamshi ya kijaahiliyyah matamshi yasiyoridhiwa na kila mwenye chembe ya iymaan, wachila mbali Muumba.

Dada yangu katika iymaan, kuomboleza kijahili iwe kwa kujipiga piga mashavu au sehemu yoyote ile katika mwili, kujinyoa nywele au kuzivuta, kuchana nguo, kukwaruza uso na kujiapiza au kutamka matamshi ya kijaahiliyyah na maajabu ya dunia ikiwemo kujiombea mauti ni moja kati ya desturi na kawaida za kijahiliyyah ambazo bado zina nafasi kubwa katika baadhi ya nafsi za wengi miongoni mwa wenye kujiita Waislamu hasa wa kike wakisahau kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhadharisha na kutuwekea wazi uwazi wa mwangaza wa mchana kuwa ulimi –kupayuka kwetu- ndio unaopelekea kuadhibiwa au kurehemewa, hivyo tuchague lenye kheri nasi na kwa maiti wetu; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah Haadhibu kwa chozi la jicho, na wala kwa huzuni za moyo, lakini Huadhibu kwa huu akiashiri ulimi wake au Hurehemu…” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy; katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa kauli kwenye mgonjwa, Hadiyth namba 1228].

Dada yangu katika iymaan, katika kujaribu kuiondosha na kuing’oa desturi hii ya kijaahiliyyah Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameikemea kwa makemeo ya hali ya juu kwa kuwa huko ni kutokuridhika na kutoamini Qudra ya Muumba [nako ni kufru] na kutokuamini yaliyothibiti kwa kila aliyefikiwa na msiba akasubiri; hivyo desturi hii ya kijahili imekemewa makemeo yaliyo makali yenye kupelekea kuhakikisha kuwa kila Muislamu aliyefikiwa na msiba ajilazimishe kusubiri, subira itayompelekea kuweza kufikia kujichotea Aliyoyaandaa Allaah kwa wenye kusubiri na kuridhika na msiba uliomshukia, Mjumbe wa Allaah amefikia kusema kuwa ‘si katika sisi, kwa maana kuwa si katika Waumini’ kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Ibn Mas’uwd (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Si katika sisi mwenye kulia kwa kujipiga piga, kujichania nguo na kuomboleza kwa maombolezo ya kijaahiliyah.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Al-Janaaiz, mlango wa si katika sisi mwenye kulia kwa kujipiga piga…, Hadiyth namba 1221 na 1222; na katika Kitabu cha Al-Manaaqib, mlango yenye kukatazwa miongoni mwa maombolezo ya kijaahiliyyah, Hadiyth namba 3281; na Muslim, katika Kitabu cha Iymaan, mlango wa Uharamu wa kujipiga piga na kujichana chana nguo, Hadiyth namba 151].

Dada yangu katika iymaan, la maajabu ni kuwa mtu kuingia katika Uislamu hutarajiwa kuwa amejivua na kujing’oa na yote aliyokuwa nayo ya kijaahiliyyah vinginevyo huwa bado hakuingia katika Uislamu kikamilifu kama Alivyoamrishwa na Muumba; Allaah Anasema:

“Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu kikamilifu, na wala msifuate hatua za shaytwaan. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.” [Al-Baqarah 2: 208].

Dada yangu katika iymaan, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na ni matarajio kuwa kila mwenye kuwafuata kwa ihsaan kuwa mbali umbali wa mbingu na ardhi na hizi mila za kijaahiliyyah kama ilivyothibiti katika kauli ya mmoja wa Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa:

“Abu Muusa (Radhiya Allaah ‘anhu) alipokuwa mgonjwa taabani ghafla alizimia, na kichwa chake kikiwa katika chumba cha mwanamke katika ahli zake, basi mwanamke katika ahli zake akapiga kelele –kulia kwa sauti-, [Abu Muusa (Radhiya Allaah ‘anhu)] hakuweza kumrudi kwa chochote kile, alipozinduka, [Abuu Muusa] akasema: Mimi niko mbali –naepukana- na yale -matendo- yote aliyojiweka nayo mbali –aliyokataza na kuyakemea- Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam); kwani Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amejiweka mbali na Asw-Swaaliqah –mwanamke mwenye kulia kwa kunyanyua sauti yake na kupayuka kwa sababu ya msiba uliomshukia-, na [pia amejiweka mbali na] Al-Haaliqah –mwanamke mwenye kunyoa nywele zake kwa sababu ya msiba-, na [pia amejiweka mbali na] Ash-Shaaqah –mwanamke mwenye kupasua nguo zake sababu ya msiba-.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Iymaan, mlango wa uharamu wa kupiga piga mashavu na kuchana chana nguo, Hadiyth namba 152 na 153].

Hadiyth iko wazi kabisa katika kukataza na kukemea:
1. Kulia kwa kunyanyua sauti na kupayuka
2. Kujinyoa nywele
3. Kuchana chana nguo na kujipiga piga wakati wa msiba.

Dada yangu katika iymaan, desturi hizi - mambo matatu haya- ni katika zenye kuonekana na kudhihiri kuwa ni zenye kupendwa na ni yenye nguvu na kuwa na washabiki wengi mpaka yakaonekana kuwa ni katika mafundisho ya Uislamu kwani ni katika mambo ya kawaida na ni yenye kukubalika kuwepo katika misiba kwa kuwa yanaonekana katika karibu misiba yote; yawe ya wenye kujiita Waislamu na Waislamu wa kawaida na hata wale wenye kudhaniwa kuwa ni wenye elimu au wenye kufikiriwa kuwa wanafuata mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Dada yangu katika iymaan, na kila Muislamu mwenye kumpenda Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake kiramu (Radhiya Allaahu ‘anhum) na kuwafuata kwa ihsaan; ukiwafikishwa kuusoma na kuuelewa waraka huu, ni vyema ushikamane na ujilazimishe kushikamana na mafundisho sahihi ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maisha yako kwa ujumla na katika kila lenye kukusibu lenye kukupelekea kuhuzunika kwa kutoweka kwake au kulikosa; kwani ushauri wa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kuwa tushikamane na Sunnah zake na Sunnah za Makhalifa wake waongofu kama ilivyothibiti katika Hadiyth kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Nakuusieni kuwa na taqwah ya Allaah, na kusikiliza na kutii hata ikiwa –huyo kiongozi wenu atakayekuamrisheni- ni mtumwa wa kihabashi; kwani hakika atakaeishi miongoni mwenu baada yangu ataona –atakutana atapambana na – ikhtilafu nyingi; kwa hiyo shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa Ar-Raashidiyn Al-Mahdiyyiyn -walioongoka-, shikamaneni nazo na ziumeni kwa magego -zikamateni kwa nguvu zenu zote wala msiziache-; na tahadharini na mambo ya uzushi, kwani hakika kila uzushi ni bid'ah –uzushi katika dini-, na kila bid’ah ni upotofu.” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad wake, katika Musnad ya Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad Ash-Shamiyyiyna, Hadiyth ya Al-‘Ir-baadh bin Saariyah, Hadiyth namba 16815; na Abu Daawuud, katika Kitabu cha Sunnah, mlango katika kulazimu Sunnah, Hadiyth namba 3994; na At-Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Elimu, mlango wa yaliyokuja katika kushikamana na Sunnah na kujiepusha na bida’h, Hadiyth namba 2620].

Dada yangu katika iymaan, tusizue wala tusiige na wala tusiipambe misiba yetu mambo ya kijaahiliyyah ambayo yaliyochopekwa na kupachikwa katika mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kupambiwa Waislamu kwa lengo la kuwapoteza na kuwabaidisha na mafunzo sahihi ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); hivyo katika uhai wako wote yasikughururi yale yote yenye kufanywa na watu wasiokuwa Waislamu, na pia yale yenye kutendwa na kupigiwa debe na wale wanaojiita Waislamu ambao wako mbali na Sunnah za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na mafundisho yake sahihi katika kawaida, na katika maisha yao hufanya kila jambo lililokatazwa na shari’ah bali huzua na kumzulia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wachilia mbali unapowasibu msiba wakati ambao hutumbukia na kung’ang’ania kila lenye kuzushwa bila ya kuelewa au kujali kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutahadharisha kwa kusema:

“Atakayetenda kitendo kisichokuwa na mafunzo ya dini yetu, hicho kitarudishwa.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Al-Hajj, milango ya al Muhswir na jazaa ya kuwinda, Hadiyth namba 2513; na Muslim, katika Kitabu cha Al-Ak-dhiyyah, mlango wa kuvunja hukumu batili na kurudisha yenye kuzushwa., Hadiyth namba 3248 na 3249].

 Posted By Posted juu ya Monday, December 03 @ 23:05:04 PST na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili:
Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa Rafiki





Mada zinazohusiana

Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili

 

Ẹsin Islam الدين الإسلامي Religion of Islam Addinin Musulunci Agama Islam Religión del Islam 伊斯兰教 Dini ya Kiislamu Религия Ислам Religião do Islã イスラム教 Esin Islam 이슬람의 종교 Portal African Muslim Website - Arabic English African Islamic Website For World News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Articles, Radio, Audio, Video, Quran, Hadith, TV Channels, Fatwas, Muslim News, Newspapers, Magazines Headlines, Forums, College, Schools, Universities, Mosques, Quranic, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Ramadan, Vidoes, Books, Fasting, PDFs On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com