Swahili
- Ukurasa Kuu    - Kumi Juu    - Mada Mpya    - Salimisha Habari    - Tafuta    - Kiswahili Jukwaa    - Kiswahili Wanachama    - Tathmini    - Ujumbe wa Kibinafsi    - Tafiti    - Majarida    - Hadithi Archive    - Maudhui    - Viungo vya Wavuti    - Vipakuliwa    - Maswali ya Kawaida    - Tunapendekeze    - Orodha ya Kuingia   
 


Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU
 
Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili  Mfumo Na Muelekeo Wa Nyaraka Hizi Umechukuliwa Kutoka Kwa Kijitabu Kinachoitwa 

“Al-Mar’at Al-Muslimah Fiy Twalabil ‘Ilm”  

Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU 

 (Mwanamke Muislamu Katika Kutafuta Elimu)

Kilichochapishwa Na Daarul Arqam,  Chapa Ya Pili, 

MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU UMMUL MU’MININA ‘AISHAH BINT ABUBAKR AS-SIDDIQ: 

Alizaliwa mwaka wa 4 Baada ya Utume (614 BI). Babake alikuwa ni ‘AbdAllaah bin ‘Uthman bin ‘Aamir at-Taymi au Abu Bakr as-Siddiq bin Abi Quhafah. Mamake alikuwa Umm Ruman bint ‘Aamir bin ‘Uwaymir al-Kananiyah. ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa ni msomi, mwenye akili, uoni wa hali ya juu na uwezo wa kutatua mambo nyeti na mazito ya Dini. Alikuwa msitari wa mbele katika upokeaji wa Hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), nambari sita miongoni mwa Masahaba wote (Radhiya Allaahu ‘anhum). Amepokea Hadithi 2,220, miongoni mwa hizo 174 zikiwa ni Muttafaqun ‘alayhi, 54 katika al-Bukhari, 67 katika Muslim, na 2,017 katika vitabu vyengine vya Hadithi. Alikuwa mjuzi sana katika elimu za Qur’ani, Hadithi, Fikihi, Mashairi, Historia na Nasaba. Anahesabiwa miongoni mwa Mujtahid na jina lake linatajwabila ya shaka pamoja na yale ya Abu bakr, ‘Umar, ‘Athman, ‘Ali, Ibn Mas‘ud, Ibn ‘Abbas na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhum). Alikuwa akitoa fatwa wakati wa Abu Bakr, ‘Umar na ‘Athman.  ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa na fadhila kubwa kuliko wanawake wote. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ubora wa ‘Aishah kulinganisha na wanawake wengine ni kama ubora wa tharid kwa aina nyengine ya vyakula”.


Alikuwa mwalimu mzuri na mkubwa na alifundisha elimu kutoka kizazi kimoja mpaka chengine. Aliwafundisha wasichana, wavulana na watu wazima. Alitumia njia tofauti ya kufundisha kama kutoa muhadhara na baadae wanafunzi kuuliza maswali, mchanag’anyiko wa mazungumzo na mjadala au wakati mwengine wanafunzi walikuwa wakiuliza maswali na yeye akatoa majibu ya kina au wanafunzi na mwalimu walikuwa wakijadili bila vikwazo au pingamizi yeyote. Mayatima wa Madinah walipata uanagalizi maalumu na matumizi yao yalishughulikiwa na ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanatizamwa na kulelewa naye.

Idadi ya watu waliofaidi kutoka kwake walikuwa ni wengi. Walionawiri zaidi ni:

· ‘AbdAllaah bin Zubayr, mtoto wa dadake ‘Aishah aliyekuwa akiitwa Asmaa.
· Aswad.
· ‘Urwah bin Zubayr, aliyekuwa mtoto wa Asmaa na mdogo wa ‘AbdAllaah bin Zubayr. Huyu aliinukia kuwa mwanachuoni mkubwa Madinah.
· Qaasim bin Muhammad, mtoto wa kakake, ambaye alikuwa mwanachuoni mkubwa wa sheria.
· Abu Salamah bin ‘Abdur-Rahman, ambaye alikuwa mwanachuoni maarufu wa Hadithi.
· Masruq, kijana kutoka Iraq, ambaye baadae alikuwa mwanachuoni wa juu kabisa katika sheria huko Iraq.
· Imam Nakhai, kutoka Iraq.
· ‘Amrah bint ‘Abdur-Rahman, msichana wa Ki-Ansaar. Alikuwa msichana hodari sana, hivyo kupendwa sana na ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Hadithi zilizokusanywa wakati wa utawala wa Khalifa ‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziz zilikaguliwa na yeye.

‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alisema: “Nimepatiwa vitu ambavyo hakupatiwa mwanamke mwengine yeyote. Niliposwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikiwa miaka saba. Malaikah alimletea sura yangu mkononi mwake ili aniangalie na nilianza kukaa naye nikiwa miaka tisa. Nilimuona Jibril ('Alayhis Salaam) na nilikuwa mke niliyependwa zaidi kuliko wote. Alipokuwa mgonjwa (Mtume) na baadae kufariki, hakushuhudiwa na mwengine isipokuwa na mimi na Malaikah. Katika riwaya nyengine alisema: Hakuowa bikra ila mimi wala mwanamke wazazi wake waliohama isipokuwa mimi. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) aliteremsha kutoka mbinguni aya za kujulisha kuwa sina makosa. Wahyi ulikuwa ukiteremka nami niko naye (Mtume). Tulikuwa tunaoga kutoka chombo kimoja na alifariki katika nyumba yangu na siku yangu na akazikwa katika chumba changu”.

Kuhusu elimu yake Masruq amesema, “Nimewaona Masahaba wazee miongoni mwa wale waliokuwa wakubwa wakimuuliza kuhusu mirathi”. Naye ‘Ataa bin Abi Rabah amesema, “‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ni Fakihi mkubwa na mwenye elimu miongoni mwa watu”. Amesema Hisham bin ‘Urwah kutoka kwa babake kuwa, “Sijamuona yeyote mjuzi wa Fikihi wala utabibu wala mashairimfano wa ‘Aishah (Radhiya Allaahu ‘anha)”. Amesema Abu Burdah bin Abi Musa kutoka kwa babake kuwa, “Hatukuwa na tatizo lolote la jambo tukamuuliza ‘Aishah isipokuwa tulimpata anayo elimu kuhusu jambo hilo”.

‘Aishah aliaga dunia tarehe 17th Ramadhan 58 BH (13th Julai 678 BI) usiku wa Jumanne. Salah yake ya Jeneza iliongozwa na Abu Hurayrah. 

Wake wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa ni wataalamu wa mambo ya Dini na walikuwa wakifundisha elimu hizo na kuzisambaza. Hafsah bint ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa anajua kuandika na kusoma. Ummu Salamah Hind bint Abi Umayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipokea Hadithi nyingi na ni wa pili miongoni mwa wakeze Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

UMMU SULAYM BINT MILHAN:

Alikuwa anaitwa Rumaysaa bint Milhan bin Khalid bin Zayd bin Kiraam kutoka katika ukoo wa Khazraj. Alikuwa ni mwanamke mrembo, mwenye akili na rai mzuri, mkarimu na hodari. Kwa sifa hizi tukufu aliposwa na kuolewa na mtoto wa ami yake aliyekuwa akiitwa Malik bin nadhr na kuzaa mtoto Anas. Mwangaza wa Uislamu ulipoingia Madinah Umm Sulaym alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kusilimu. Hakujali kwa yatakayomfika. Wa mwanzo kuwa kikwazo kwake ni mumewe aliporudi safari, ambaye alimghadhibikia lakini yeye hakujali. Alimsilimisha mtoto wao mbele ya mumewe. Mumewe akawa anamwambia usimharibu mtoto wangu, lakini alijibu kuwa yeye anamfundisha adabu na nidhamu.

Mume alipoona kuwa mkewe ana azma ya nguvu kuliko mwamba alitoka nyumbani na huku amekasirika na hapo kukutwa na adui yake na kuuliwa. Baada ya hapo alimpeleka mtoto wake Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku anaona haya na kumtaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amchukue mtoto wake ili amtumikie. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimkubali na watu wakawa wanahadithia kuhusu Anas na mamake kwa ajabu. Abu Talhah aliposikia habari ya kufa kwa mumewe alienda ili kutaka kumposa kwa mali nyingi, lakini Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) alikataa kwa kuwa yeye ni kafiri. Abu Talhah alikuja siku ya pili na kutaka kutoa mali zaidi. Lakini Daa‘iyah Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) mbali na kuona mali mbele yake, jaha na ubarobaro alikataa kwa kusema: “Naapa kwa Allaah! Mfano wako ewe Abu Talhah hawarudishwi. Lakini wewe ni mtu kafiri na mimi ni mwanamke Muislamu. Haifai kwangu kuolewa na wewe, lakini unaposilimu tu hayo yatakuwa mahari yangu na wala sitakuuliza kitu chengine”.

Abu Talhah alishangazwa na maneno haya kwa kuona kuwa Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) si mwanamke wa kuchezewa. Yeye alikuwa ni mwanamke mwenye akili ambaye anakataa kuvutiwa na dunia. Hakujitambua ila ulimi wake unarudia shahadah. Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) akamuangalia mtoto wake, Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) nae anasema kwa utukufu mkubwa kuwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amemuongoza Abu Takhah kupitia kwa mkono wake. Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisimama hapo kumuoza Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mamake. Kwa hayo alisema Thabit rawi wa Hadithi kutoka kwa Anas: “Sijasikia kabisa mwanamke aliyekuwa na mahari matukufu na ya ukarimu kuliko Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha). Mahari yake yalikuwa Uislamu”.

Aliishi Ummu Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) na Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) maisha ya ndoa yaliyosimama juu ya msimamo wa Kiislamu ambao umewapatia dhamana mume na mke maisha ya utulivu na mazuri. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Aliwapatia mtoto ambaye kuja kwake kulileta furaha na wakampatia jina Aba ‘Umayr. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Akawapatia mtihani kwa kumchukua mtoto mzuri waliompenda baada ya kuwa mgonjwa kwa muda. Wakati huo babake alikuwa amekwenda Msikitini. Mama huyu muumini alikubali matokeo haya kwa kusubiri na huku ameridhika kwa kusema: “Tunatoka kwa Allaah na Kwake tutarudi”. Aliwaambia watu wake, “Musimpashe Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) mpaka mimi mwenyewe ni muelezee habari hiyo ya kifo”.

Aliporudi Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu), machozi ya rehema ya Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) tayari yalikuwa yamekauka na alikuwa tayari kumpokea mumewe na kujibu maswali yake. Aliuliza, “Je, mtoto yu hali gani?” Akasema, “Yuko katyika hali bora kabisa”. Akadhania kwa utulivu na raha ya mkewe kuwa mtoto yu salama. Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) alimletea mumewe chakula na kuvaa nguo mzuri kabisa, akajipamba na kujipaka manukato. Mumewe alipojitosheleza naye alimshukuru Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Ilipofika mwisho wa usiku alisema, “Ewe Abu Talhah! Waonaje ikiwa watu wamekukopesha kisha wakahitaji amana yao. Je, utawanyima?” akasema, “La!” Akasema tena, “Utasema nini watakapo gawa nusu na kutaka amana yao baada ya kufaidika nayo”. Akasema, “Hawakufanya haki”. Akasema, “Hakika mtoto wako ulikuwa ni mkopo kutoka kwa Allaah na Amemchukua”. Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) hakuweza kumiliki yaliyomsibu, hivyo kusema kwa hasira: “Umeniacha mpaka nilipoingiwa na doa ndipo uliponieleza kuhusu mtoto wangu”. Aliendelea kumkumbuka mpaka aliporudi Nyuma na kumshukuru Allaah na nafsi yake kutulia. Kulipopambazuka alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumhadithia yaliyotokea. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Allaah awabariki kwa usiku wenu”. Huo ndio usiku wa kushika mimba Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) na kuzaliwa kwa ‘AbdAllaah bin Abi Talhah. Alipozaliwa alipatiwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) ampeleke kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitia tende mdomoni na ilipokuwa laini akamtilia mdomoni mwa mtoto. Akasema Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu), “Mpatie jina ewe Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)”. Akasema, “Yeye ni ‘AbdAllaah”. Alisema ‘Ubabah mmoja wa watu katika isnadi, hakika nimewaona watoto wa huyu kijana wote wakiwa wamehifadhi Qur’ani.

Juu ya mama huyu mtukufu na mumewe muumini, Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) aliteremsha aya ambayo watu wataisoma mpaka Siku ya Mwisho. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, “Alikuwa mtu muhitaji na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na chochote katika nyumba zake. Akasema: ‘Nani atakayemkirimu mgeni huyu Allaah atamrehemu’. Abu Talhah (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema, ‘Mimi ewe Mjumbe wa Allaah’. Alipofika kwa mkewe (Umm Sulaym) alimuuliza, ‘Je, una chochote?’ Akasema, ‘La! Isipokuwa chakula cha watoto’. Akasema: ‘Wapumbaze na vitu mpaka walale. Atakapoingia mgeni wetu tumuonyeshe kama tunakula. Atakapoanza kula inuka ufanye kama unatengeneza taa kishe uizime’. Naye alifanya hivyo na mgeni akala mpaka akashiba na wao pamoja na watoto wakalala na njaa. Alipoamka alikwenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alimwambia: ‘Hakika Allaah Ameona ajabu - au Allaah amefurahi na Fulani (mume) na Fulani (mke)”. Katika riwaya nyengine: “Allaah amestaajabu kwa kitendo chenu kwa mgeni wenu wa usiku. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Akateremsha aya inayosema: 

‘…Na wanawapendelea kuliko nafsi zao ingawa wenyewe wana hali ndogo”.

Ummu Sulaym (Radhiya Allaaha ‘anhu) alikuwa na daraja kubwa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye hakuwa akienda nyumba nyengine yeyote isipokuwa yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimbashiria pepo aliposema: “Niliingia Peponi nikasikia sauti ya viatu. Nikasema nani huyu? Nikaambiwa, huyu ni Rumaisaa bint Milhan, mamake Anas bin Malik”.

Pongezi kwako ewe Umm Sulaym (Radhiya Allaahu ‘anha) kwani unastahiki yote hayo. Ulikuwa mke mwema mwenye kutoa nasaha njema na Daa‘iyah mwenye hekima na mama mlezi mwenye muamko. Ulimuingiza mtoto wako katika Madrasa bora na kubwa zaidi iliyojulikana na ulimwengu, Madrasa ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye hajafika hata miaka kumi. Na kwa hivyo akawa mwananchuoni miongoni mwa wanavyuoni wa Uislamu. 

SHAFAA’ BINT ABDALLAAH:

Ummu Sulayman Shafaa’ bint ‘AbdAllaah bin al-Harith, alikuwa Mqureshi katika ukoo wa ‘Adiy. Alisilimu kabla ya Hijrah na miongoni mwa watu wa mwanzo kuhama Madinah. Pia alikuwa miongoni mwa Waumini waliombai (kumuahidi) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliotajwa katika Qur’ani Tukufu. Alikuwa mwanamke mwenye akili na mbora wao na msomi miongoni mwa wasomi wa Kiislamu. Alikuwa na elimu nyingi na Imani.

Aliolewa na Abu Hathmah bin Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kutunukiwa mtoto aliyeitwa Sulayman. Shafaa’ (Radhiya Allaahu ‘anhu) alijifundisha kusoma na kuandika alipokuwa Makkah na kabla ya kusilimu. Aliposilimu aliwafundisha Waislamu wanawake akitarajia thawabu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Kwa kazi hiyo akawa mwalimu wa kike wa kwanza wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Miongoni mwa wanafunzi wake ni Hafsah bint ‘Umar al-Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu), mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Inafahamika kuwa Shafaa’ alikuwa akifanya ruqyah wakati wa Ujahiliyyah. Aliposilimu alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu jambo hilo na kumuonyesha alivyokuwa akifanya. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimruhusu kuendelea na kumuambia amfundishe Hafsah.

Alijifunza Hadithi nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa akiita watu katika Uislamu na kutoa nasaha kwa wote. Wamepokea kutoka kwake mtoto wake Sulayman, wajukuu zake AbuBakr na ‘Uthman bin Sulayman, Abu Salamah bin Abdur-Rahman, hafsah Ummul Mu’minina na mjakazi wake Abu Ishaaq. ‘Umar bin al-Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akimtanguliza katika rai, akimtaka ushauri na kumheshimu. Pia alimtawalisha idara ya kuangalia mambo ya masoko. Naye alikuwa akimheshimu ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Alikuwa mkweli, kiigizo kizuri katika kusuluhisha, Uchaji Mwenyeezi Mungu na uadilifu. Siku moja aliwaona vijana wanatembea pole pole na wanazungumza kwa taratibu. Akasema: “Hii ni nini?” Wakasema: “Huu ni utawa”. Akasema: “Naapa kwa Allaah! Alikuwa ‘Umar anapozungumza anasikika na anapotembea anakwenda haraka na anapopiga anaumiza”. 

Aliaga dunia mwaka wa 20 BH. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amrehemu kwani aliutumikia Ummah huu katika mambo ya kheri. Anatakikana awe kielelezo chema kwa wasichana ili nao wasiwe mabakhili kwa kuitoa elimu waliyo nayo na kuwafundisha wengine katika njia ya Itikadi ya kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala).

MIFANO MENGINE:

Asmaa bint Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mtu wa kumi na saba kusilimu na kumbai Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamuamini Imani ya nguvu. Mamake alikuwa akiitwa Qatilah bint ‘Abdul ‘Izzy. Alipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na babake wanahama, yeyepamoja na kuwa mja mzito alikuwa akiwapelekea chakula katika Pango la Thaur. Alipata adha mkononi mwa adui wa Allaah, Abu Jahl ambaye alikuja nyumbani na kuuliza: “Kenda wapi babako?” aliposema kuwa hajui, Abu Jahl alimzaba kofi la uso, hata vipuli vyake vikamdondoka na uso ukamwiva mwekundu. Hivi ndivyo wanavyofanya waoga kila zama, wakishindwa kuwapiga na kuwaua wanaume wanawapiga wanawake na watoto.

Ndiye muhaji wa kwanza wa kike kuzaa Madinah mtoto aliyeitwa ‘AbdAllaah. Mumewe alikuwa ni Zubayr bin Awwam (Radhiya Allaahu ‘anhu). Alikuwa shujaa asiyeogopa kitu katika njia ya Allaah. Wakati mtoto wake ‘AbdAllaah alipouliwa na Hajjaj bin Yusuf Makkah na mwili wake kusulubiwa, Hajjaj alikwenda kwa Asmaa na kumwambia: “Ewe mamangu! Hakika Amirul Mu’minin ameniusia juu yako. Je, una haja ya chochote?” Akasema: “Mimi si mama yako, lakini mama wa aliyesulubiwa. Nami sina haja, lakini ninakuhadithia kuwa nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ‘Atatoka kutoka Thaqeef mwongona mharabu’. Ama muongo tumemuona (akimaanisha Mukhtar na ama mharabu ni wewe”. Katika riwaya nyengine zinaeleza kuwa Hajjaj alipoingia kwa Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alimwambia: “Umeonaje jinsi nilivyomfanya mtoto wako, ewe Asmaa?” Akasema kwa utulivu: “Umeiharibu dunia yake, na yeye ameiharibu Akhera (mwisho) wako”.

Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alikufa siku chache baada ya kuuliwa mtoto wake ‘AbdAllaah (Radhiya Allaahu ‘anhu), Mfungo Nane (Jamadil Awwal) mwka 73 BH hapo Makkah. Alikufa akiwa mzee lakini hakutoa jino hata moja wala hakupoteza akili. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amrehemu kwani alikuwa mfano mzuri wa ushujaa na subira.

Tunapata mfano wa Ummul Kulthum bint ‘Ali bin Abu Talib (Radhiya Allaahu ‘anhu), ambaye alikuwa mke wa Khalifa wa pili, ‘Umar bin al-Khattab (Radhiya Allaahu ‘anhu) walipokwenda usiku wa manane kuwahudumia mume na mkewe aliyekuwa na uchungu wa kuzaa.

Sumayyah bint Khayyat (Radhiya Allaahu ‘anha) ni mfano wa mwanamke aliyesilimu mikononi mwa mtoto wake ‘Ammar (Radhiya Allaahu ‘anhu). hapo ulianza mtihani kwa familia ya mama huyu ya kuteswa na kuadhibiwa lakini waote walisimama imara. Abu Jahl kuona uimara wa Sumayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) alimuua kutumia mkuki na roho yake safi yenye Imani ikatoka. Hapo akawa shahidi wa kwanza katika Ummah huu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hapa tunapata mfano mwema wa utukufu, ushujaa, istiqamah na Imani na kujitolea mhanga kwa kufa katika njia ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala).

Mfano mwengine ni Asmaa bint yazeed bin as-Sakan katika ukoo wa Aws. Alikuwa mzungumzaji mzuri, mujahidah mtukufu, mwenye akili na ufahamu wa dini na khatibah mpaka akaitwa khatibah wa wanawake. Kama wanawake wengi waliohitimu katika madrassah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawakujua kujisalimisha katika maneno, wala kukubali udhalilifu wa kuzama kwa cheo bali walikuwa na ushujaa, uthabiti na uimara na juhudi walizowaletea mabanati jinsi yao mfano katika kila nyanja. Alikuwa akisikiliza Hadithi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hakuogopa wala kuona haya kuuliza maswali hata yakiwa nyeti namna gani katika mambo ya dini. Yeye ndiye aliyeuliza njia ya kujitahirisha kwa mwanamke na hedhi.

Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa akiwakilisha wanawake katika kuzungumza na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mara moja alikuja na kusema: “Ewe Mtume wa Allaah! Mimi ni mjumbe Nyuma yangu kuna kundi la wanawake Waislamu wote wanasema ninayo yasema. Na wao wana mfano wa rai yangu … Hakika Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amekutumiliza kwa wanaume na wanawake, tumekuamini na kukufuata. Na sisi kongamano la wanawake tuna upungufu, tunakaa majumbani mwetu na sehemu ya kuwatimizia matamanio wanaume zetu na kuwabebea watoto wao. Wanaume wana fadhila kwa kuhudhuria jamaa, kushuhudia janaza na jihadi. Wakitoka kueleke katika jihadi tunawahifadhia mali zao na tunawalea watoto wao. Je, tutashirikiana katika thawabu, ewe Mtume wa Allaah?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwazungukia Masahaba zake na kusema: “Mumesikia maneno ya mwanamke. Je, kuna suali lililo bora zaidi katika dini yake kuliko hili?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema tena: “Ewe Asmaa! Nenda uwaambie wanawake walio Nyuma yako ni bora mmoja wenu akae vizuri na mumewe katika Maisha ya ndoa na kutaka radhi yake na kufuata anayoyataka basi hayo yatakuwa sawa na mambo yote uliyoyataja ya wanaume”. Akaondoka Asmaa (Radhiya Allaahu ‘anha) na huku anatoa tahlil na takbir kutoa bishara njema kwa aliyo yasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Alishiriki katika vya vya Yarmuk na kuwaua Warumi tisa kwa kutumia kipande cha hema. Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) amrehemu kwa juhudi zake kwa zile Hadithi alizozipokea na zile darasa muhimu tulizopata kutoka kwake kwa kutoona haya katika kuuliza masuala ya haki na ya dini. Alifariki mwaka 30 BH>

Umm Hiram bint Milhan (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa miongoni mwa Ansaar. Anasema Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anakwenda Quba alikuwa alikuwa akiingia kwa Umm Hiram ((Radhiya Allaahu ‘anha) na kula. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa mke wa Ubadah bin Saamit (Radhiya Allaahu ‘anhu). Siku moja alikwenda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na baada ya kula akajinyosha na kulala. Baadae aliamka na huku anacheka. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema, ‘Ni kipi kinacho kuchekesha ewe Mtume wa Allaah?’ Akasema, ‘Watu katika Ummah wangu wameonyeshwa kwangu wakipigana katika njia ya Allaah. Wamepanda meli kwenye bahari kubwa mfano wa wafalme juu ya mateka’.

Akasema Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha), ‘Ewe Mtume wa Allaah! Niombee kwa Allaah niwe miongoni mwao”. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuombea kisha akalala tena, lakini akaamka tena na huku anacheka. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) akasema: “Ewe Mtume wa Allaah ni kipi kinacho kuchekesha?” Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Nimeonyeshwa watu katika Ummah wangu wakipigana katika njia ya Allaah mfano wa wafalme juu ya mateka’. Akasema: ‘Ewe Mtume wa Allaah! Niombee Allaah niwe pamoja nao’. Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Wewe uko pamoja na wale wa mwanzo’. Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) akasema: Alitoka Umm Hirama pamoja na mumewe na walipofika baharini, meli ilipanda mnyama na kuvunjika naye akaaga dunia. Hivyo vilikuwa Vita vya Cyprus na akazikwa hapo. Amiri wa jeshi hilo alikuwa ni Mu‘awiyah bin Abi Sufyan (Radhiya Allaahu ‘anhu) katika Ukhalifa wa ‘Uthman (Radhiya Allaahu ‘anhu)”. Huo ulikuwa ni mwaka wa 27 BH. Umm Hiram (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa shahidi wa kwanza wa bahari.

Bila pia kuusahau mfano wa Tamadhir bint ‘Amr bin al-Harith (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni maarufu kwa jina Khansaa. Alikuwa mshairi mkubwa. Wakati wa Vita vya al-Qadisiyyah wakati wa Ukhalifa wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwakusanya watoto wake wanne usiku ili kuwaelekeza na kuwahimiza wapigane kishujaa katika vita na wasirudi Nyuma. 

Aliwafanya wapende kufa mashahidi katika njia ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Hebu tupulikize wasiya wake mwema, alipowaambia: Enyi watoto wangu! Nyinyi mumesilimu kwa kupenda kwenu na mulichagua kuhama. Naapa kwa Allaah, Ambaye hapana Mola ila Yeye kuwa nyinyi ni watoto wa mwanamke mmoja. Baba yenu hakufanya hiyana wala halati yenu hakuleta fedheha wala sikuchang’anya nasaba yenu wala sikubadilisha ukoo wenu. Nyinyi mnajua aliyowaandalia Allaah Waislamu kwa thawabu kubwa katika kupigana na makafiri. Na jueni kuwa nyumba yenye kubaki ni bora kuliko nyumba yenye kuondoka. Amesema Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala): ‘Enyi Mlioamini! Subirini na muwashinde makafiri (katika kusubiri), na kuweni imara (nyoyo zenu) na mcheni Allaah ili mpate kufuzu’. Mutakapo amka kesho InshaAllaah mukiwa salama jiandaeni kupigana na adui kwa uoni, hamasa na kwa hamu. Na Allaah Atawapatia nusra juu ya maadui.

Mutakapoona vita vimeshamiri juu ya miguu na kuwaka moto wa kufululiza na moto kufinika njia za kupitia basi tieni nia ya kufanya bidii na mpigeni raisi wao kwa kuukata ushujaa wake, mutashinda kwa kupata ghanima (ngawira) na utukufu wa milele na cheo…” Siku ya vita vijana wote walipigana kwa ushujaa na wote wakafa mashahidi. Habari ilipomfikia mama Muumini mwenye kusubiri, hakubabika, hakuhuzunika wala hakulia juu yao bali alisema maneno yake mashuhuri ambayo historia yameyanukuu na kuyarudia. Haya maneno yatabaki kurudiwa mpaka atakapo penda Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Alisema: “Sifa zote njema anastahiki Allaah ambaye amenitukuza kwa kuwapatia Shahada. Naomba kwa Mola wangu anijumuishe nao katika makao ya rehema Yake”.

‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliutambua ubora wa Khansaa na watoto wake (Radhiya Allaahu ‘anha), hivyo kuendelea kumpatia sehemu ya chakula cha watoto wake mpaka alipofariki. Khansaa (Radhiya Allaahu ‘anha) alikufa jangwani mwaka 24 BH, mwanzo wa kipindi cha Ukhalifa wa ‘Uthman (Radhiya Allaahu ‘anhu). Huu ni mfano mwema wa subira na malezi mazuri kwa watoto na kutoa nasaha ambazo kila mwanamke anatakiwa aige. Naye alipatiwa jina la Umm Shuhadaa (mama wa mashahidi). 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwabashiria wanawake ishirini Pepo kama alivyowabashiria wanaume kumi. Hawa wanawake walipata bishara hiyo kwa dauru kubwa waliocheza katika kuutetea na kuutumikia Uislamu. Nao ni Khadijah bint Khuwaylid, ‘Aishah bint AbuBakr, Hafsah bint ‘Umar, Zaynab bint Jahsh [hawa wanne walikuwa wake za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)], Fatimah bint Rasuul, al-Fari‘ah bint Malik, Ummu Mundhir bint Qays, Asmaa bint AbuBakr, Ummu Sulaym bint Milhan, Ummu Hiram bint Milhan, Ummu Waraqah bint ‘AbdAllaah al-Ansariyah, Asmaa bint Yazeed, Umm Hisham bint Haarithah, Fatimah bint Asad, Ummu ‘Ammarah Nusaybah bint Ka‘b, Ummu Ruuman Zaynab (au Da‘d) bint ‘Aamir, Barakah bint Tha‘labah, ar-Rabi‘ bint Mu‘awwadh, Sumayyah bint Khabbat na Kabshah bint Raafi‘.

Hii ni baadhii ya mifano ya wanawake watukufu waliotuachia kielelezo kizuri cha sisi kufuata. Wametuonyesha mwangaza katika giza la usiku na kutufundisha mengi lau tutayatilia maanani basi tutafaulu hapa duniani na kesho Akhera. Wametuachia mifano katika kutafuta elimu na kusomesha, katika biashara na kufanya kazi, katika nyanja zote za Jihadi na malezi ya watoto. Walicheza dauru yao muhimu na kuwaachia wanawake majukumu lau watayatekeleza basi tuhma zote dhidi ya mwanamke wa Kiislamu zitaondoka na maendeleo yatapatikana.

HITIMISHO 

Hakika mwanamke Muislamu mwenye muamko, msomi na mwalimu, ni mtu anayejenga na mfanya kazi ni miongoni mwa wafanya kheri na anayeleta baraka kwa Ummah huu. Na huenda akasema msemaji kuwa bila shaka elimu leo, tunamshukuru Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) imeenea sana na kiwango cha wenye elimu ni kikubwa na ujinga ni mchache sana ikiwa haupo kabisa.

Lakini mwenye kuangalia elimu iliyozagaa leo anaona elimu iliyo karibu kwa maana ya elimu ya kuandika na kusoma pekee. Laiti ingekuwa katika daraja ya juu ya kisomo na usahihi. Je, hiyo ndiyo elimu ambayo itajenga Ummah? Dkt. An-Nafeesy amesema katika kitabu chake ukurasa wa 17: “Napenda kusajili hapa kuwa masomo peke yake huenda yasiwe ni hatua ya kusonga mbele katika haki ya mwanafunzi. Mara nyingi haya hutegemea maumbile ya mfumo wa elimu na masomo na dhamana ya kijamii, kisiasa na kiitikadi”
Hivyo, ikiwa masomo yamejazwa na fikra za kimagharibi haitotumikia Uislamu hata ikiwa watamaliza mamia na maelfu kila mwaka na wala haimanishi kuwa hiyo ndiyo elimu inayohitajika na kuimbiwa. 

Elimu zote kwa ujumla zikiwa zinaleta kheri kwa wanadamu, sisi tutazipokea bila kujali nchi zinazotoka au kabila walizozitoa. Kizazi cha kwanza cha Ummah huu wamechukua elimu za mataifa mbali mbali zilizopita. Lakini wao walizibadilisha katika muelekeo wa Kiislamu na wakazihami na Itikadi, maadili na adabu tukufu. Kwa njia hiyo, ustaarabu huo wa Kiislamu ulitoa matunda ulioangaza mashariki na magharibi ya ardhi. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza sana kuwa busara na elimu ni haki ya Muislamu pale aliposema: “Hekima ni kitu kilichompotea Muislamu, popote anapoipata ana haki zaidi (kuichukua)”.

Kwa hivyo ni wajibu wa dada Muislamu katika kutafuta elimu ajiepushe na athari za utamaduni wa kimagharibi au kujaalia kutokana na elimu kuwa ni njia ya kupata kazi katika hali zote. Leo tunaona kuwa elimu imechkuliwa kuwa njia ya kuandikwa kazi. Msichana anayepata Shahada (cheti) bila kupata kazi anahasirika katika masomo yake na umri wake ambao ameutumia bila ya kupata matunda. Muelekeo huu unawafanya watoto wetu (wavulana na wasichana) kuwa ni watu wa masikio ya kazi. Hawafikirii Misingi kwani elimu katika mipaka yao ni lengo wala sio njia. Kisha, bila shaka elimu katika zama hizi za sasa ni mtihani wa balaa wenye athari ya mbali na hatari kubwa. Hatari hii ni ya mchang’anyiko baina ya wasichana na wavulana na mambo haya ni wajibu tusifuate na tuwalinde vijana na hatari zake.

Sayyid Rahmatullah Hashemi amesema: “Hatuna shida (yaani serikali ya Taliban) yeyote na elimu ya wanawake. Tumesema tunataka elimu… kwani hiyo ni sehemu ya Itikadi yetu. Tumeamrishwa kufanya hivyo … Ni kweli kuwa tunapinga mchang’anyiko katika elimu lakini si kweli kuwa tunapinga elimu ya wanawake. Hivi karibuni tumefungua kitengo cha utabibu katika miji yote mikubwa ya Afghanistan na Kandahar. Wako wasichana wengi zaidi wanaosoma katika kitengo cha utabibu kuliko wavulana”.

Mwisho kabisa tunataka wasichana wa Kiislamu watie niya upya katika kutafuta elimu ili iwe hiyo niya kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) pekee. Lengo la kusoma liwe ni kuleta muamko na kujenga dola ya Kiislamu na kuleta faida katika kila nyanja na fani tofauti. Yote haya yatekelezwe kwa kutaka radhi za Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala), Aliyesema: 
“Sema: ‘Je, wanaweza kuwa wale wanaojua na wale wasiojua? Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu”.

Waingereza wana msemo unaosema: “When you teach a woman, you teach the family (Unapomfundisha mwanamke, umeifundisha familia)”. Na Mshairi mmoja wa Kiarabu amesema: “Mama ni Madrasa, ukimuandaa umeandaa jamii mzima.”

 Posted By Posted juu ya Saturday, March 09 @ 17:06:20 PST na MediaSwahiliTeam
 

Comments 💬 التعليقات
 

For Your Membership Comments And Registered Debates Please, See Below Or Register Here :-: للحصول على تعليقات عضويتك و مناقشات الأعضاء انظر من فضلك أدناه أو سجّل هنا

Kuhusiana Viungo

· zaidi Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili
· Habari na MediaSwahiliTeam


Kweli kusoma hadithi kuhusu Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili:
Elimu Ni Wajibu Kwa Mwanamke Wa Kiislamu - MIFANO YA WANAWAKE WATUKUFU


Kifungu Rating

Wastani matokeo: 0
Kura: 0

Tafadhali chukua ya pili na kupiga kura kwa ajili ya makala hii:

bora
Vizuri Sana
Mema
Kawaidar
Mbaya


Chaguzi


 Chapa Rafiki Chapa Rafiki





Mada zinazohusiana

Waislamu Wanawake - maisha yao na Famili

 

Ẹsin Islam الدين الإسلامي Religion of Islam Addinin Musulunci Agama Islam Religión del Islam 伊斯兰教 Dini ya Kiislamu Религия Ислам Religião do Islã イスラム教 Esin Islam 이슬람의 종교 Portal African Muslim Website - Arabic English African Islamic Website For World News, Fatwas, Audios, Videos, Muslim News, Articles, Radio, Audio, Video, Quran, Hadith, TV Channels, Fatwas, Muslim News, Newspapers, Magazines Headlines, Forums, College, Schools, Universities, Mosques, Quranic, Sunnah, Fiqh, Prayers, Salat, Ramadan, Vidoes, Books, Fasting, PDFs On EsinIslam.Com And IslamAfrica.Com