Na tukazitia nguvu nyoyo zao walipo simama na wakasema: Mola wetu Mlezi ni Mola
Mlezi wa mbingu na ardhi. Hatutamwita mwenginewe kabisa badala yake kuwa ni
Mungu. Hivyo itakuwa tumesema jambo la kuvuka mpaka.
Hawa watu wetu wameshika miungu mingine badala yake Yeye. Kwa nini basi
hawawatolei uthibitisho ulio dhaahiri? Na nani aliye dhaalimu zaidi kuliko anaye
mzulia uwongo Mwenyezi Mungu?
Na mkijitenga nao na vile wanavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu, basi
kimbilieni pangoni, akufungulieni Mola wenu Mlezi rehema yake, na
akutengenezeeni ya kukufaeni katika mambo yenu.
Na unaliona jua linapo chomoza linainamia kuliani mwao kutoka hapo pangoni; na
linapo kuchwa linawakwepa kushotoni, na wao wamo katika uwazi wa pango. Hizo ni
katika ishara za Mwenyezi Mungu. Ambaye Mwenyezi Mungu anamwongoa basi huyo ni
mwenye kuongoka. Na anaye muacha kupotea basi hutampatia mlinzi wala mwongozi.
Nawe utawadhania wamacho, na hali wamelala. Nasi tunawageuza kulia na kushoto.
Na mbwa wao amenyoosha miguu yake ya mbele kizingitini. Kama ungeli watokea
hapana shaka ungeli geuka kuwakimbia, nawe umejaa khofu.
Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema
msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya
siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja
wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora
kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala
asikutajeni kabisa kwa yeyote.
Na namna hivi tuliwa juulisha kwa watu wapate kujua ya kwamba ahadi ya Mwenyezi
Mungu ni ya kweli, na kwamba Saa haina shaka. Walipo kuwa wakigombania jambo lao
wao kwa wao walisema: Jengeni jengo juu yao. Mola wao Mlezi anawajua vyema.
Wakasema walio shinda katika shauri yao: Bila ya shaka tutawajengea msikiti juu
yao.
Watasema: Walikuwa watatu, wa nne wao ni mbwa wao. Na wanasema: Walikuwa watano,
wa sita wao ni mbwa wao. Wanavurumisha ovyo. Na wanasema: Walikuwa saba, na wa
nane wao ni mbwa wao. Sema: Mola wangu Mlezi ndiye anaye jua sawa sawa hisabu
yao. Hawawajui ila wachache tu. Basi usibishane juu yao ila kwa mabishano ya juu
juu tu hivi. Wala usiulize khabari zao kwa yeyote yule.
Isipo kuwa Mwenyezi Mungu akipenda. Na mkumbuke Mola wako Mlezi pale unapo
sahau, na sema: Asaa Mola wangu Mlezi ataniongoa kwenye uwongozi ulio karibu
zaidi kuliko huu.
Sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi muda walio kaa. Ni zake tu siri za mbingu na
ardhi. Kuona kulioje na kusikia kwake! Hawana mlinzi isipo kuwa Yeye, wala
hamshirikishi yeyote katika hukumu yake.
Na isubirishe nafsi yako pamoja na wanao muomba Mola wao Mlezi asubuhi na jioni,
hali ya kuwa wanataka radhi yake. Wala macho yako yasiwaruke kwa kutaka pambo la
maisha ya dunia. Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na
akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka.
Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na
atakaye, akatae. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu Moto ambao
utawazunguka kama khema. Na wakiomba msaada watasaidiwa kwa kupewa maji kama
mafuta yaliyo tibuka. Yatayo wababua nyuso zao. Kinywaji hicho ni kiovu mno! Na
matandiko hayo ya kupumzikia ni maovu mno!
Hao watapata Bustani za milele, zinazo pita mito kati yake. Humo watapambwa kwa
mavazi ya mikononi ya dhahabu, na watavaa nguo za kijani za hariri na at'ilasi,
huku wakiegemea humo juu ya makochi. Ni malipo bora hayo! Na matandiko mazuri
mno ya kupumzikia!
Na lau kuwa ulipo ingia kitaluni kwako ungeli sema: Mashaallah! Alitakalo
Mwenyezi Mungu huwa! Hapana nguvu ila kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa unaniona mimi
nina mali kidogo na watoto kuliko wewe,
Basi huenda Mola wangu Mlezi akanipa kilicho bora kuliko kitalu chako, naye
akapitisha kudra yake kutoka mbinguni kukilitea hicho chako, na kikageuka ardhi
tupu inayo teleza.
Yakateketezwa matunda yake, akabaki akipindua pindua viganja vyake, kwa vile
alivyo yagharimia, na miti imebwagika juu ya chanja zake. Akawa anasema: Laiti
nisingeli mshiriki Mola wangu Mlezi na yeyote!
Na wapigie mfano wa maisha ya dunia. Hayo ni kama maji tunayo yateremsha kutoka
mbinguni, yakachanganyika na mimea ya ardhi, kisha hiyo mimea ikawa vibuwa
vinavyo peperushwa na upepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
Na wakahudhurishwa mbele ya Mola wako Mlezi kwa safu (wakaambiwa): Mmetujia kama
tulivyo kuumbeni mara ya kwanza! Bali mlidai kwamba hatutakuwekeeni miadi.
Na kitawekwa kitabu. Basi utawaona wakosefu wanavyo ogopa kwa yale yaliomo humo.
Na watasema: Ole wetu! Kitabu hichi kina nini! Hakiachi dogo wala kubwa ila
huliandika? Na watayakuta yote waliyo yatenda yamehudhuria hapo. Na Mola wako
Mlezi hamdhulumu yeyote.
Na tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam! Walimsjudia isipo kuwa Iblisi. Yeye
alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja amri ya Mola wake Mlezi. Je! Mnamshika
yeye na dhuriya zake kuwa marafiki badala yangu, hali wao ni adui zenu? Ni ovu
mno badala hii kwa wenye kudhulumu.
Na siku atakapo sema (Mwenyezi Mungu): Waiteni hao mlio dai kuwa ni washirika
wangu. Basi watawaita, na wao hawato waitikia. Nasi tutaweka baina yao
maangamio.
Na hapana kilicho wazuia watu kuamini ulipo wajia uwongofu na wakaomba maghfira
kwa Mola wao Mlezi, isipo kuwa yawafikie ya wale wa zamani, au iwafikie adhabu
jahara.
Na hatuwatumi Mitume ila wawe wabashiri na waonyaji. Na walio kufuru wanabishana
kwa uwongo, ili kwa uwongo huo waivunje kweli. Na wanazifanya Ishara zangu na
yale waliyo onywa kuwa ni mzaha.
Na ni nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye kumbushwa Ishara za Mola wake
Mlezi, naye akazipuuza na akasahau yaliyo tangulizwa na mikono yake? Hakika Sisi
tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao ili wasifahamu, na uziwi kwenye masikio yao.
Na ukiwaita kwenye uwongofu hawakubali kabisa kuongoka.
Na Mola wako Mlezi ni Msamehevu Mwenye rehema. Lau angeli wachukulia kwa mujibu
waliyo yachuma, bila ya shaka angeli wafanyia haraka kuwaadhibu. Lakini wanayo
miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya kuepukana nayo.
Akasema (kijana): Waona! Pale tulipo pumzika penye jabali basi mimi nilimsahau
yule samaki. Na hapana aliye nisahaulisha nisimkumbuke ila Shet'ani tu. Naye
akashika njia yake baharini kwa ajabu.
Basi wakatoka wawili hao mpaka wakamkuta kijana, akamuuwa. (Musa) akasema: Ala!
Umemuuwa mtu asiye na kosa, na wala hakuuwa! Ama hakika umefanya jambo baya
kabisa!
Basi wakatoka mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja. Wakawaomba watu wake wawape
chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka,
(yule mja mwema) akausimamisha. (Musa) akasema: Ungeli taka ungeli chukua ujira
kwa haya.
Na ama ukuta, huo ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini. Na chini yake
ilikuwako khazina yao; na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako Mlezi
alitaka wafikie utu uzima na wajitolee khazina yao wenyewe, kuwa ni rehema
itokayo kwa Mola wako Mlezi. Wala mimi sikutenda hayo kwa amri yangu. Hiyo ndiyo
tafsiri ya hayo ambayo wewe hukuweza kuyasubiria.
Hata alipo fika machwea-jua aliliona linatua katika checmchem yenye matope
meusi. Na hapo akawakuta watu. Tukasema: Ewe Dhul-Qarnaini! Ama uwaadhibu au
watwae kwa wema.
Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipo ijaza nafasi iliyo kati ya milima
miwili, akasema: Vukuteni. Hata alipo kifanya (chuma) kama moto akasema:
Nileteeni shaba iliyo yayuka niimwagie.
Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu Mlezi. Na itapo fika ahadi ya Mola
wangu Mlezi atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu Mlezi ni kweli tu.
Je, wanadhani walio kufuru ndio wawafanye waja wangu ndio walinzi wao badala
yangu Mimi? Hakika Sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ndipo mahala pa kuteremkia
makafiri.
Hao ni wale walio zikanusha Ishara za Mola wao Mlezi na kukutana naye. Kwa hivyo
vitendo vyao vimepotea bure, na wala Siku ya Kiyama hatutawathamini kitu.
Sema: Lau kuwa bahari ndio wino kwa maneno ya Mola wangu Mlezi, basi bahari
ingeli malizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu Mlezi, hata tungeli
ileta mfano wa hiyo kuongezea.
Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi. Ninaletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni
Mungu Mmoja. Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi naatende vitendo
vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake Mlezi.