Na wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo tuitia, na masikio
yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe lipo pazia. Basi wewe tenda, nasi
tunatenda.
Sema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni
Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake msamaha, na ole
wao wanao mshirikisha,
Kisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na ardhi: Njooni,
kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni wat'iifu.
Basi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na akazipangia kila mbingu mambo
yake. Na tukaipamba mbingu ya chini kwa mataa na kwa ulinzi. Hichi ndicho kipimo
cha Mwenyezi Mungu Mwenye Kujua.
Walipo wajia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi
Mungu! Wakasema: Angeli taka Mola wetu Mlezi bila ya shaka angeli wateremsha
Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyo tumwa.
Ama kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye kuwa
na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba
ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!
Basi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za ukorofi, ili tuwaonjeshe
adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina
hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
Na ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walipenda upofu kuliko uwongofu. Basi
uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyo kuwa
wakiyachuma.
Na wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo zitasema:
Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliye
kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa.
Na hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu,
zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika
mliyo kuwa mkiyatenda.
Na tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao. Basi
ikawathibitikia kauli wawe pamoja na mataifa yaliyo pita kabla yao, miongoni mwa
majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kukhasirika.
Hayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na maskani
ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.
Na walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe walio tupoteza miongoni mwa
majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni wa walio
chini kabisa.
Na katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua
wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu
Yeye tu.
Na katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge, lakini tunapo iteremshia
maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliye ihuisha ardhi
ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Hakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii Sisi.
Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama?
Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda.
Na lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema: Kwanini Aya zake
haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani
ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo uziwi katika masikio
yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali.
Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea khitilafu kati yake. Na lau kuwa
halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo
katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu
basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu
waja.
UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu Mwenyezi Mungu. Na matunda
hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai, ila kwa
kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako wapi washirika wangu? Hapo
watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni mwetu anaye shuhudia hayo.
Na pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa dhara, bila ya
shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na hata
nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina mema yangu kwake! Basi kwa
yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda, na kwa yakini
tutawaonjesha adhabu ngumu.
Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka
iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa
Yeye ni Shahidi wa kila kitu?