Enyi mlio amini! Timizeni ahadi. Mmehalalishiwa wanyama wa mifugo, ila wale mnao
tajiwa. Lakini msihalalishe kuwinda nanyi mmo katika Hija. Hakika Mwenyezi Mungu
anahukumu apendavyo.
Enyi mlio amini! Msivunje hishima ya alama ya Dini ya Mwenyezi Mungu wala mwezi
mtakatifu, wala wanyama wanao pelekwa Makka kuchinjwa, wala vigwe vyao, wala
wanao elekea kwendea Nyumba Takatifu, wakitafuta fadhila na radhi za Mola wao
Mlezi. Na mkisha toka Hija yenu basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa
wali- kuzuilieni kufika Msikiti mtakatifu kusikupelekeeni kuwafanyia uadui. Na
saidianeni katika wema na uchamngu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na
mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliye chinjwa si
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na aliye kufa kwa kunyongeka koo, na aliye kufa kwa
kupigwa, na aliye kufa kwa kuanguka, na aliye kufa kwa kupigwa pembe, aliye liwa
na mnyama, ila mkimdiriki kumchinja. Na pia ni haramu kula nyama aliye chinjiwa
masanamu. Na ni haramu kupiga ramli. Hayo yote ni upotovu. Leo walio kufuru
wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo
nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na
nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini. Na mwenye kushurutishwa na njaa, bila
ya kupendelea dhambi, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye
kurehemu.
Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri na
mlicho wafundisha wanyama kukiwinda. Mnawafundisha alivyo kufunzeni Mwenyezi
Mungu. Basi kuleni walicho kukamatieni, na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu. Na
mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni
halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa
Waumini, na wanawake wema miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, mtakapo
wapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka
kinyumba. Na anaye kataa kuamini bila shaka a'mali yake imepotea, naye katika
Akhera atakuwa miongoni mwa wenye khasara.
Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na
mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka
vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au
mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi
tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi
Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza
neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.
Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, na ahadi yake aliyo
fungamana nanyi mlipo sema: Tumesikia na tumet'ii. Na mcheni Mwenyezi Mungu.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyomo vifuani.
Enyi mlio amini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mkitoa
ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu.
Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamngu. Na mcheni Mwenyezi
Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Enyi mlio amini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, walipo taka
watu kukunyooshieni mikono, naye akaizuilia mikono yao kukufikieni. Na mcheni
Mwenyezi Mungu. Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.
Na Mwenyezi Mungu alifanya agano na Wana wa Israili. Na tukawateulia kutokana
nao wakuu kumi na mbili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa yakini Mimi ni pamoja
nanyi. Mkisali, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na
mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, hapana shaka nitakufutieni maovu yenu na
nitakuingizeni katika mabustani yapitayo mito kati yake. Lakini atakaye kufuru
miongoni mwenu baada ya hayo bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa.
Basi kwa sababu ya kuvunja agano lao tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa
ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahala pake, na wamesahau sehemu ya yale
waliyo kumbushwa. Na huachi kuvumbua khiana kutokana nao, isipo kuwa wachache
miongoni mwao. Basi wasamehe na waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao
wema.
Na kutoka kwa wale walio sema: Sisi ni Manasara, tulichukua ahadi yao, lakini
wakasahau sehemu ya waliyo kumbushwa. Kwa hivyo tukaweka kati yao uadui na chuki
mpaka Siku ya Kiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia waliyo kuwa wakiyafanya.
Enyi Watu wa Kitabu! Amekwisha kujieni Mtume wetu anaye kufichulieni mengi mliyo
kuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anaye samehe mengi. Bila shaka imekujieni
kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kinacho bainisha.
Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na
huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye
njia iliyo nyooka.
Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu. Sema:
Ni nani mwenye kumiliki cho chote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka
kumuangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika
ardhi? Na mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi
Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu.
Na Mayahudi na Wakristo wanasema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi
vyake. Sema: Basi kwa nini anakuadhibuni kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi
ni watu tu kama wale wengine alio waumba. Humsamehe amtakaye na humuadhibu
amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni
kwake Yeye.
Enyi Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amekujilieni Mtume wetu akikubainishieni
katika wakati usio kuwa na Mitume, msije mkasema: Hakufika kwetu mbashiri wala
mwonyaji. Basi amekujieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu anao uweza wa
kila kitu.
Na pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za
Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipo wateuwa Manabii kati yenu, na akakufanyeni
watawala, na akakupeni ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu.
Watu wawili miongoni mwa wachamngu ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, walisema:
Waingilieni kwa mlangoni. Mtakapo waingilia basi kwa yakini nyinyi mtashinda. Na
mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi nchi hiyo wameharimishiwa muda wa miaka arubaini,
watakuwa wakitanga-tanga katika ardhi. Basi wewe usiwasikitikie watu wapotovu.
Na wasomee khabari za wana wawili wa Adam kwa kweli. Walipo toa mhanga,
ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwengine haukukubaliwa. Akasema: Nitakuuwa.
Akasema mwengine: Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu.
Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anaye fukua katika ardhi ili amwonyeshe
vipi kumsitiri nduguye. Akasema: Ole wangu! Nimeshindwa kuwa kama kunguru huyu
nikamsitiri ndugu yangu? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta.
Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila
ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote.
Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia
Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa
waharibifu katika nchi.
Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania
kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao
na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika
dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa.
Hakika walio kufuru lau wange kuwa na yote yaliyomo duniani, na mengine kama
hayo, ili watoe fidia ya kuepukana na adhabu ya Siku ya Kiyama, yasingeli
pokelewa kwao; na watapata adhabu chungu.
Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, hayo ni malipo ya
waliyo yachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Lakini mwenye kutubia baada ya dhulma yake, na akatengenea, basi Mwenyezi Mungu
atapokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wa fanyao haraka kukufuru, miongoni mwa wanao sema
kwa vinywa vyao: Tumeamini, na hali nyoyo zao hazikuamini, na miongoni mwa
Mayahudi, wanao sikiliza kwa ajili ya uwongo, wanao sikiliza kwa ajili ya watu
wengine wasio kufikia. Wao huyabadilisha maneno kutoka pahala pake. Wanasema:
Mkipewa haya basi yashikeni, na msipo pewa haya tahadharini. Na mtu ambaye
Mwenyezi Mungu anataka kumfitini huwezi kuwa na madaraka naye mbele ya Mwenyezi
Mungu. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzitakasa nyoyo zao. Watakuwa na
hizaya duniani, na Akhera watakuwa na adhabu kubwa.
Hao ni wasikilizaji kwa ajili ya kusema uwongo, na ni walaji mno vya haramu!
Basi wakikujia, wahukumu baina yao au jipuuze nao. Na ukijipuuza nao, basi wao
hawatakudhuru kitu. Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika
Mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu.
Hakika Sisi tuliteremsha Taurati yenye uwongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii
walio nyenyekea kiislamu, na wachamngu, na wanazuoni, waliwahukumu Mayahudi;
kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni
mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali niogopeni Mimi. Wala msibadilishe
Aya zangu kwa thamani chache. Na wasio hukumu kwa aliyo teremsha Mwenyezi Mungu,
basi hao ndio makafiri.
Na humo tuliwaandikia ya kwamba roho kwa roho, na jicho kwa jicho, na pua kwa
pua, na sikio kwa sikio, na jino kwa jino, na kwa majaraha kisasi. Lakini
atakaye samehe basi itakuwa ni kafara kwake. Na wasio hukumu kwa yale aliyo
yateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhaalimu.
Na tukawafuatishia hao Isa bin Maryamu kuyahakikisha yaliyo kuwa kabla yake
katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uwongofu, na nuru na inayo
sadikisha yaliyo kuwa kabla yake katika Taurati, na uwongofu na mawaidha kwa
wachamngu.
Na wahukumu Watu wa Injili kwa yale aliyo teremsha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na
wasio hukumu kwa yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio wapotofu.
Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, Kitabu hichi kinacho sadikisha yaliyo kuwa
kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa aliyo
yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha Haki iliyo kujia.
Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sharia yake na njia yake. Na lau kuwa
Mwenyezi Mungu angeli taka ange kufanyeni nyote umma mmoja, lakini ni
kukujaribuni kwa aliyo kupeni. Basi shindaneni kwa mambo ya kheri. Kwa Mwenyezi
Mungu ndio marejeo yenu nyote, na atakuja kuwaambieni yale mliyo kuwa
mkikhitalifiana.
Na wahukumu baina yao kwa aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate
matamanio yao. Nawe tahadhari nao wasije kukufitini ukaacha baadhi ya aliyo
kuteremshia Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi jua kwamba hakika Mwenyezi Mungu
anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na hakika wengi wa watu ni wapotofu.
Enyi mlio amini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa ni marafiki. Wao ni
marafiki wao kwa wao. Na miongoni mwenu mwenye kufanya urafiki nao, basi huyo ni
katika wao. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu.
Na walio amini watasema: Hivyo hawa ndio wale walio apa ukomo wa viapo vyao kuwa
wao wa pamoja nanyi? Vitendo vyao vitapotea bure, na wataamkia kuwa wenye
kukhasirika.
Enyi mlio amini! Atakaye iacha miongoni mwenu Dini yake, basi Mwenyezi Mungu
atakuja leta watu anao wapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye
nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala
hawaogopi lawama ya anaye laumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa
amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na Mwenye kujua.
Enyi mlio amini! Msiwafanye marafiki wale walio ifanyia kejeli na mchezo Dini
yenu miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, na makafiri wengine. Na mcheni
Mwenyezi Mungu kama nyinyi ni wenye kuamini.
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hivyo mnatuchukia kwa kuwa tumemuamini Mwenyezi Mungu
na tuliyo teremshiwa na yaliyo teremshwa kabla, na kwa kuwa wengi katika nyinyi
ni wapotofu?
Sema: Je! Nikwambieni yule ambaye ni mwenye malipo mabaya zaidi kuliko hayo
mbele ya Mwenyezi Mungu? Ni yule ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani na
amemkasirikia, na amewafanya miongoni mwao manyani na nguruwe, na wakamuabudu
Shet'ani. Hao ndio wenye mahali pabaya na wamepotea zaidi njia iliyo sawa.
Na wanapo kujieni husema: Tumeamini. Lakini hakika wao wameingia na ukafiri wao,
na wametoka nao pia. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi kabisa wa yote wanayo yaficha.
Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndiyo iliyo
fumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyo yasema. Bali mikono yake iwazi. Hutoa
apendavyo. Kwa yakini yaliyo teremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi
yatawazidisha wengi katika wao uasi na kufuru. Na Sisi tumewatilia uadui na
chuki baina yao mpaka Siku ya Kiyama. Kila mara wanapo washa moto wa vita,
Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi. Na
Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu.
Na lau kuwa wangeli ishika Taurati na Injili na yote waliyo teremshiwa kutokana
na Mola wao Mlezi, basi hapana shaka wangeli kula vya juu yao na vya chini ya
miguu yao. Wapo watu miongoni mwao walio sawa, lakini wengi wao wanayo yafanya
ni mabaya mno.
Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa
hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na
watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hamna lenu jambo mpaka muishike Taurati na Injili na
yote mlio teremshiwa kutokana na Mola wenu Mlezi. Na hakika ulio teremshiwa wewe
kutokana na Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na ukafiri.
Basi usiwasikitikie watu makafiri.
Hakika walio amini, na Mayahudi na Masabii na Wakristo, walio muamini Mwenyezi
Mungu, na Siku ya mwisho, na wakatenda mema, basi hawatakuwa na khofu wala
hawatahuzunika.
Tulifanya agano na Wana wa Israili, na tukawatumia Mitume. Kila alipo wajia
Mtume kwa wasio yapenda nafsi zao wengine waliwakanusha na wengine wakawauwa.
Na wakadhani kuwa hapatakuwa majaribio; basi wakawa vipofu na viziwi. Kisha
Mwenyezi Mungu akawapokelea toba zao. Kisha tena wengi katika wao wakawa vipofu
na viziwi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona hayo wayatendayo.
Hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryamu! Na hali
Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola
wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika
Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na walio dhulumu
hawatakuwa na wa kuwanusuru.
Kwa hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa Utatu. Hali
hakuna mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayo yasema, kwa yakini
itawakamata adhabu chungu wale wanao kufuru.
Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume. Wamekwisha pita Mitume kabla
yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula.
Angalia jinsi tunavyo wabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyo geuzwa.
Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu bila ya haki. Wala
msifuate matamanio ya watu walio kwisha potea tangu zamani, na wakawapoteza
wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa.
Walilaaniwa walio kufuru miongoni mwa Wana wa Israili kwa ulimi wa Daud na wa
Isa mwana wa Maryamu. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapindukia mipaka.
Utawaona wengi wao wanafanya urafiki na walio kufuru. Hakika ni maovu yaliyo
tangulizwa na nafsi zao hata Mwenyezi Mungu amewakasirikia, nao watadumu katika
adhabu.
Na lau wangeli kuwa wanamuamini Mwenyezi Mungu, na huyu Nabii, na yaliyo
teremshwa kwake, wasingeli wafanya hao marafiki. Lakini wengi katika wao ni
wapotofu.
Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika uadui kwa walio amini ni
Mayahudi na washirikina. Na utawakuta walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanao
sema: Sisi ni Manasara. Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na
wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi.
NA WANAPO SIKIA yaliyo teremshwa kwa Mtume utaona macho yao yanachururika
machozi kwa sababu ya Haki waliyo itambua. Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini.
Basi tuandike pamoja na wanao shuhudia.
Mwenyezi Mungu hatakushikeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakushikeni kwa
mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini
kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuwavisha, au
kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya
viapo vyenu mnapo apa. Na hifadhini yamini zenu. Namna hivyo Mwenyezi Mungu
anakubainishieni Aya zake ili mpate kushukuru.
Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga
ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate
kufanikiwa.
Si dhambi juu ya walio amini na wakatenda mema kwa walivyo vila (zamani) maadamu
wakichamngu na wakiamini na wakitenda mema, kisha wakachamngu, na wakaamini,
kisha wakachamngu na wakafanya mazuri. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao
mazuri.
Enyi mlio amini! Mwenyezi Mungu atakujaribuni kidogo kwa wanyama wa kuwinda
inayo wafikia mikono yenu na mikuki yenu, ili Mwenyezi Mungu amjue nani anaye
mkhofu kwa ghaibu. Basi atakaye ruka mipaka baada ya hayo atapata adhabu kali.
Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi mmeharimia katika Hija. Na
miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja
kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu
wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al Kaaba, au kutoa kafara kwa
kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake
hili. Mwenyezi Mungu amekwisha yafuta yaliyo pita; lakini atakaye fanya tena
Mwenyezi Mungu atampa adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye
kuadhibu.
Nyinyi mmehalalishiwa kuvua vinyama vya baharini na kuvila, kwa faida yenu na
kwa wasafiri. Na mmeharimishiwa mawindo ya wanyama wa bara maadamu mmeharimia
Hija. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mtakusanywa kwake.
Mwenyezi Mungu ameifanya Al Kaaba, hii Nyumba Tukufu, ni simamio la watu, na
kadhaalika Miezi Mitukufu, na wanyama wa dhabihu, na vigwe. Hayo ili mjue ya
kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na yaliyomo katika ardhi, na ya
kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Enyi mlio amini! Msiulize mambo ambayo mkidhihirishiwa yatakuchukizeni. Na
mkiyauliza inapo teremshwa Qur'ani mtabainishiwa. Mwenyezi Mungu amesamehe hayo.
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira Mpole.
Mwenyezi Mungu hakujaalia uharamu wowote juu ya "Bahira" wala "Saiba" wala
"Wasila" wala "Hami". Lakini walio kufuru humzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na
wengi wao hawatumii akili.
Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, na kwa
Mtume, husema: Yanatutosha tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao
walikuwa hawajui kitu wala hawakuongoka?
Enyi mlio amini! Kilicho lazima juu yenu ni nafsi zenu. Hawakudhuruni walio
potoka ikiwa nyinyi mmeongoka. Ni kwa Mwenyezi Mungu ndio marudio yenu nyote;
basi atakwambieni yale mliyo kuwa mkiyatenda.
Enyi mlio amini! Yanapo mfikia mauti mmoja wenu na akataka kutoa wasia, basi
wawepo mashahidi wawili miongoni mwenu ambao ni waadilifu. Na mnapo kuwa
safarini, na msiba wa mauti ukakusibuni, basi washuhudie wengineo wawili wasio
kuwa katika nyinyi. Mtawazuia wawili hao baada ya Sala na waape kwa Mwenyezi
Mungu, mkitilia shaka, wakisema: Hatutopokea thamani yoyote kwa haya hata kwa
ajili ya jamaa; na wala hatutaficha ushahidi wa Mwenyezi Mungu; hakika hapo
tutakuwa miongoni mwa wenye dhambi.
Ikigundulikana kuwa wawili hao wamestahiki dhambi, basi wawili wengineo kutokana
na warithi wenye kudai haki washike makamo ya wa mwanzo. Nao waape kwa Mwenyezi
Mungu wakisema: Hakika ushahidi wetu ni wa haki zaidi kuliko ushahidi wa wale.
Na sisi hatujafanya dhambi; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa walio dhulumu.
Hivi inaelekea zaidi ya kwamba watatoa ushahidi ulio sawa au wataogopa visije
vikaletwa viapo vingine baada ya viapo vyao. Na mcheni Mwenyezi Mungu na msikie.
Na hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi wapotofu.
Ile siku ambayo Mwenyezi Mungu atapo wakusanya Mitume awaambie: Mlijibiwa nini?
Watasema: Hatuna ujuzi; hakika Wewe ndiye Mjuzi Mkubwa wa yote yaliyo fichikana.
Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu
yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu, ukazungumza na
watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na
Taurati na Injili. Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu,
kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na
wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo
kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio
kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu!
Wanafunzi walipo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Je, Mola wako Mlezi anaweza
kututeremshia chakula kutoka mbinguni? Akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa
nyinyi ni Waumini.
Akasema Isa bin Maryamu: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshia
chakula kutoka mbinguni ili kiwe Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa
mwisho wetu, na kiwe ni Ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye
mbora wa wanao ruzuku.
Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitakuteremshieni hicho. Lakini yeyote
katika nyinyi atakaye kanya baadae, basi hakika Mimi nitampa adhabu nisiyopata
kumpa yeyote katika walimwengu.
Na pale Mwenyezi Mungu atakapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Ati wewe uliwaambia
watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu? (Na
Isa) atasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki
yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo
ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe
ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyo fichikana.
Sikuwaambia lolote ila uliyo niamrisha, nayo ni: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola
wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipo kuwa
nao. Na ulipo nifisha ukawa Wewe ndiye Muangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi
juu ya kila kitu.
Mwenyezi Mungu atasema: Hii ndiyo Siku ambayo wasemao kweli utawafaa ukweli wao.
Wao watapata Bustani zipitazo mito kati yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi
Mungu amewawia radhi, nao wawe radhi naye. Huku ndiko kufuzu kukubwa.