Na miongoni mwa watu wapo wanao nunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na
njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata
adhabu ya kuwafedhehesha.
Na (mtu kama huyo) anapo somewa Aya zetu huzipa mgongo kwa kujivuna, kama kwamba
hakuzisikia, kama kwamba masikioni mwake mna uziwi. Basi mbashirie kuwa atapata
adhabu chungu.
Ameziumba mbingu bila ya nguzo mnazo ziona; na ameweka katika ardhi milima ili
ardhi isikuyumbisheni; na ametawanya humo kila namna ya wanyama; na tumeteremsha
maji kutoka mbinguni, na tukaotesha katika ardhi mimea mizuri ya kila namna.
Na tulimpa Luqman hikima, tukamwambia: Mshukuru Mwenyezi Mungu. Na mwenye
kushukuru basi hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake. Na aliye kufuru,
basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Msifiwa.
Na Luqman alipo mwambia mwanawe kwa kumpa mawaidha: Ewe mwanangu! Usimshirikishe
Mwenyezi Mungu. Kwani hakika ushirikina bila ya shaka ni dhulma iliyo kubwa.
Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa
udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia):
Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio.
Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi
usiwat'ii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anaye elekea
kwangu. Kisha marejeo yenu ni kwangu Mimi, na Mimi nitakuambieni mliyo kuwa
mkiyatenda.
Ewe mwanangu! Kikiwapo kitu cha uzito wa chembe ya khardali kikawa ndani ya
jabali au ndani ya mbingu au ndani ya ardhi, basi Mwenyezi Mungu atakileta.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyo fichika, Mwenye khabari za yote.
Kwani hamwoni ya kwamba Mwenyezi Mungu amevifanya vikutumikieni viliomo mbinguni
na kwenye ardhi, na akakujalizieni neema zake, za dhaahiri na za siri? Na
miongoni mwa watu wapo wanao bishana juu ya Mwenyezi Mungu pasipo ilimu, wala
uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.
Na wanapo ambiwa: Fuateni aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, husema: Bali
tunafuata tuliyo wakuta nayo baba zetu. Je! Ijapo kuwa Shet'ani anawaita kwenye
adhabu ya Moto uwakao?
Na mwenye kuuelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa anafanya wema, basi
huyo hakika amekwisha kamata fundo lilio madhubuti. Na mwisho wa mambo yote ni
kwa Mwenyezi Mungu.
Na anaye kufuru, isikuhuzunishe kufuru yake. Kwetu ndio marudio yao, na hapo
tutawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema:
Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.
Lakini wengi wao hawajui.
Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino),
na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli
kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu huuingiza usiku katika mchana, na huuingiza
mchana katika usiku, na amedhalilisha jua na mwezi? Vyote hivyo vinakwenda mpaka
wakati ulio wekwa. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
Hivi ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na hakika wanacho
kiomba ni cha uwongo. Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mtukufu na ndiye
Mkubwa.
Kwani huoni kwamba marikebu hupita baharini zikichukua neema za Mwenyezi Mungu,
ili kukuonyesheni baadhi ya Ishara zake? Hakika katika haya zipo Ishara kwa kila
mwenye kusubiri, mwenye kushukuru.
Na wimbi linapo wafunika kama wingu, wao humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumsafia
dini. Lakini anapo waokoa wakafika nchi kavu, wapo baadhi yao huenda mwendo wa
sawa. Wala hazikanushi Ishara zetu ila aliye khaini kafiri mkubwa.
Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi, na iogopeni siku ambayo mzazi hatamfaa mwana,
wala mwana hatamfaa mzazi kwa lolote. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya
kweli. Basi yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala asikudanganyeni na Mwenyezi
Mungu mdanganyifu.
Hakika kuijua Saa (ya Kiyama) kuko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye ndiye anaye
iteremsha mvua. Na anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi
yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika
Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari.