Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini mnaniudhi, nanyi
mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliye tumwa kwenu? Walipo
potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke. Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu wapotovu.
Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa
Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati,
na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad!
Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri!
Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu
uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu
madhaalimu.
Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni Jihadi katika Njia ya
Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi
mnajua.
Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika Mabustani yapitiwayo na mito
kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu
kukubwa.
Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyo sema Isa bin
Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu?
Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu! Basi taifa moja la Wana
wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walio
amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.