Enyi mlio amini! Msiwafanye adui zangu na adui zenu kuwa marafiki mkiwapa
mapenzi, na hali wao wamekwisha ikataa haki iliyo kujieni, wakamfukuza Mtume na
nyinyi kwa sababu mnamuamini Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu. Mnapotoka kwa
ajili ya Jihadi katika Njia yangu na kutafuta radhi yangu, mnafanya urafiki nao
kwa siri, na Mimi nayajua mnayo yaficha na mnayo dhihirisha. Na mwenye kufanya
hayo kati yenu basi ameipotea njia ya sawa.
Hakika nyinyi mna mfano mzuri kwenu kwa Ibrahim na wale walio kuwa pamoja naye,
walipo waambia watu wao: Hakika sisi tumejitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu
badala ya Mwenyezi Mungu. Tunakukataeni; na umekwisha dhihiri uadui na chuki
baina yetu na nyinyi mpaka mtakapo muamini Mwenyezi Mungu peke yake. Isipo kuwa
kauli ya Ibrahim kumwambia baba yake: Hakika nitakuombea msamaha, wala similiki
chochote kwa ajili yako mbele ya Mwenyezi Mungu. Mola wetu Mlezi! Juu yako
tumetegemea, na kwako tumeelekea, na kwako ndio marejeo.
Kwa yakini umekuwa mfano mzuri kwenu katika mwendo wao, kwa anaye mtarajia
Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na mwenye kugeuka basi hakika Mwnyezi Mungu ni
Mwenye kujitosha, Msifiwa.
Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao
hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda
wafanyao uadilifu.
Hakika Mwenyezi Mungu anakukatazeni kufanya urafiki na wale walio kupigeni vita,
na wakakutoeni makwenu, na wakasaidia katika kufukuzwa kwenu. Na wanao wafanya
hao marafiki basi hao ndio madhaalimu.
Enyi mlio amini! Wakikujilieni wanawake Waumini walio hama, basi wafanyieni
mtihani - Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua zaidi Imani yao. Mkiwa mnawajua kuwa
ni Waumini basi msiwarudishe kwa makafiri. Wanawake hao si halali kwa hao
makafiri, wala hao makafiri hawahalalikii wanawake Waumini. Na wapeni hao
wanaume mahari walio toa. Wala hapana makosa kwenu kuwaoa mkiwapa mahari yao.
Wala msiwaweke wanawake makafiri katika kifungo cha ndoa zenu. Na takeni mlicho
kitoa, na wao watake walicho kitoa. Hiyo ndiyo hukumu ya Mwenyezi Mungu anayo
kuhukumuni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hikima.
Na akitoroka yeyote katika wake zenu kwenda kwa makafiri, tena ikatokea mkapata
ngawira, basi wapeni walio kimbiwa na wake zao kiasi cha mahari waliyo yatoa. Na
mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mnamuamini.
Ewe Nabii! Watakapo kujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba
hawatamshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote, wala hawataiba, wala hawatazini,
wala hawatawauwa watoto wao, wala hawataleta uzushi wanao uzua tu wenyewe baina
ya mikono yao na miguu yao, wala hawatakuasi katika jambo jema, basi peana nao
ahadi, na uwatakie maghfira kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi
maghfira, Mwenye kurehemu.
Enyi mlio amini! Msiwafanye rafiki zenu watu ambao Mwenyezi Mungu
amewakasirikia. Hao wamekwisha kata tamaa ya Akhera, kama makafiri walivyo
wakatia tamaa watu wa makaburini.