Yeye ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu katika nyumba
zao wakati wa uhamisho wa kwanza. Hamkudhani kuwa watatoka, nao walidhani kuwa
ngome zao zitawalinda na Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu aliwafikia kwa
mahali wasipo patazamia, na akatia woga katika nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa
nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi zingatieni enyi wenye
macho!
Na mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuyakimbilia
mbio kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa mamlaka Mitume wake
juu ya wowote awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
Mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni
kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya Mtume, na jamaa, na mayatima, na
masikini, na msafiri, ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni
mwenu. Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho.
Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
Wapewe mafakiri Wahajiri walio tolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya
kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli.
Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao,
wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali
wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye
kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.
Na walio kuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu
walio tutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walio
amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu.
Huwaoni wanao fanya unaafiki wanawaambia ndugu zao walio kufuru katika Watu wa
Kitabu: Mkitolewa na sisi lazima tutatoka pamoja nanyi, wala hatutamt'ii yeyote
kabisa dhidi yenu. Na mkipigwa vita lazima tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu
anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni waongo.
Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipo kuwa katika vijiji vilivyo zatitiwa kwa
ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako
pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na
akili.
Ni kama mfano wa Shetani anapo mwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi
si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu
wote.
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza
kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo
khabari ya mnayo yatenda.
Lau kuwa tumeiteremsha hii Qur'ani juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeli uona
ukinyenyekea, ukipasuka kwa khofu ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo mifano tunawapigia
watu ili wafikiri.
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mwenye
kuyajua yaliyo fichikana na yanayo onekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye
kurehemu.
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme,
Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo
yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu
na hayo wanayo mshirikisha nayo.
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina
mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye
kushinda, Mwenye hikima.