Ewe Nabii! Kwa nini unaharimisha alicho kuhalilishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta
kuwaridhi wake zako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
Na Nabii alipo mwambia mmoja wa wake zake jambo la siri. Basi alipo litangaza
yule mke, na Mwenyezi Mungu akamdhihirishia Mtume, alimjuvya sehemu na akaacha
sehemu nyengine. Alipo mwambia hayo, huyo mke akasema: Nani aliye kwambia haya?
Mtume akasema: Kaniambia Mjuzi Mwenye khabari zote!
Kama nyinyi wawili hamkutubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwisha
elekea huko. Na mkisaidiana dhidi yake (Mtume), basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye
kipenzi chake, na Jibrili, na Waumini wema, na zaidi ya hayo Malaika pia
watasaidia.
Asaa Mola wake Mlezi, akikupeni talaka, akampa wake wengine badala yenu nyinyi,
walio bora kuliko nyinyi, wanynyekevu, Waumini, wat'awa, walio tubu, wenye
kushika ibada, wafanyao kheri, wajane na wanawari.
Enyi mlio amini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu na Moto ambao kuni zake ni
watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu
kwa anayo waamrisha, na wanatenda wanayo amrishwa.
Enyi mlio amini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu
Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati
yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii na walio amini pamoja
naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku wanasema: Mola
wetu Mlezi! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza
juu ya kila kitu.
Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walio kufuru: mke wa Nuhu na mke wa Lut'i.
Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu. Lakini
wakawakhuni waume zao, nao wasiwafae kitu. Na ikasemwa: Ingieni Motoni pamoja na
wanao ingia!
Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walio amini - mkewe Firauni, alipo sema: Mola
wangu Mlezi! Nijengee kwako nyumba Peponi, na uniokoe na Firauni na vitendo
vyake, na uniokoe na watu madhaalimu.
Na Mariamu binti wa Imrani, aliye linda ubikira wake, na tukampulizia humo
kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi na Vitabu vyake, na
alikuwa miongoni mwa wat'iifu.