Na kadhaalika Mola wako Mlezi atakuteuwa na atakufundisha tafsiri ya mambo. Na
atatimiza neema zake juu yako na juu ya ukoo wa Yaa'qub, kama alivyo watimizia
hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni Mjuzi Mwenye
hikima.
Pale walipo sema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko
sisi, hali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotofu wa
dhaahiri.
Basi walipo mchukua na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, tulimfunulia
Yusuf: Hapana shaka yoyote utakuja waambia kwa jambo lao hili, na wala wao
hawatambui.
Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana na tukamwacha Yusuf penye
vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini wewe hutuamini ijapo kuwa tunasema
kweli.
Wakaja na kanzu yake ina damu ya uwongo. Akasema: Bali nafsi zenu
zimekushawishini kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu
ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayo yaeleza.
Ukafika msafara, wakamtuma mchota maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake.
Alisema: Kheri Inshallah! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili kumfanya ni bidhaa.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayo yatenda.
Na yule aliye mnunua huko Misri alimwambia mkewe: Mtengenezee makaazi ya hishima
huyu; huenda akatufaa au tukamfanya mwenetu. Na kama hivyo tulimweka Yusuf
katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye
kushinda katika jambo lake, lakini watu wengi hawajui.
Na yule bibi wa nyumba aliyo kuwamo Yusuf alimtamani kinyume cha nafsi yake, na
akafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema: Audhubillahi! Najikinga na
Mwenyezi Mungu. Huyu bwana wangu kaniweka maskani nzuri, na hakika wenye
kudhulumu hawatengenekewi.
Na hakika yule mwanamke alimtamani, na Yusuf angeli mtamani lau kuwa hakuona
ishara ya Mola wake Mlezi. Hayo hivyo ni kwa ajili tumuepushe na uovu na uchafu.
Hakika yeye alikuwa katika waja wetu walio safishwa.
Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akairarua kanzu yake Yusuf kwa
nyuma. Na wakamkuta bwana wake mlangoni. Mwanamke akasema: Hapana malipo ya
mwenye kutaka kumfanyia maovu mkeo isipo kuwa kufungwa au kupewa adhabu chungu.
Yusuf akasema: Yeye ndiye aliye nitaka bila ya mimi kumtaka. Na shahidi aliye
kuwa katika jamaa za mwanamke alisema: Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele basi
mwanamke amesema kweli, naye Yusuf ni katika waongo.
Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa Mheshimiwa anamtamani mtumishi wake
! Hakika amesalitika kwa mapenzi. Sisi hakika tunamwona yumo katika upotovu ulio
dhaahiri.
Alipo sikia yule bibi masengenyo yao aliwaita, na akawawekea matakia ya
kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu. Akamwambia Yusuf: Tokeza mbele yao.
Basi walipo mwona waliona ni kitu kikubwa kabisa, na wakajikata mikono yao.
Wakasema: Hasha Lillahi! Huyu si mwanaadamu. Hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu.
Yule bibi aksema: Huyu basi ndiye huyo mliye nilaumia! Na kweli mimi nilimtaka
naye akakataa. Na akitofanya ninayo muamrisha basi hapana shaka atafungwa
gerezani, na atakuwa miongoni mwa walio chini kabisa.
Yusuf akasema: Ee Mola Mlezi wangu! Nastahabu kifungo kuliko haya anayo niitia.
Na usipo niondoshea vitimbi vya wanawake mimi nitamili kwao, na nitakuwa katika
wajinga.
Wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi
nimeota nakamua mvinyo. Na mwingine akasema: Mimi nimeota nimebeba mikate juu ya
kichwa changu, na ndege wanaila. Hebu tuambie tafsiri yake, kwani sisi tunakuona
wewe ni katika watu wema.
Akasema: Hakitakufikilieni chakula mtakacho pewa ila nitakwambieni hakika yake
kabla hakijakufikieni. Haya ni katika yale aliyo nifundisha Mola wangu Mlezi.
Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasio muamini Mwenyezi Mungu, na wakawa
hawaiamini Akhera.
Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Is-haq, na Yaa'qub. Hatuna haki ya
kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi
Mungu juu yetu na juu ya watu; lakini watu wengi hawashukuru.
Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga nyinyi na baba zenu. Mwenyezi
Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi
Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipo kuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini
Iliyo Nyooka. Lakini watu wengi hawajui.
Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu atamnywesha bwana wake mvinyo. Na
ama mwengine atasulubiwa, na ndege watamla kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu
ya hilo jambo mlilo kuwa mkiuliza.
Na akamwambia yule aliye jua kuwa atavuka katika wale wawili: Nikumbuke kwa
bwana wako. Lakini Shet'ani alimsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi Yusuf
akakaa gerezani miaka kadhaa.
Na siku moja mfalme alisema: Hakika mimi nimeota ng'ombe saba wanene wanaliwa na
ng'ombe saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu. Enyi
waheshimiwa! Nambieni maana ya ndoto zangu, ikiwa nyinyi mnaweza kuagua ndoto.
Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe
saba walio konda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu, ili nirejee kwa
watu wapate kujua.
Mfalme alisema: Mlikuwa mna nini mlipo mtaka Yusuf kinyume na nafsi yake?
Wakasema: Hasha Lillahi! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa Mheshimiwa
akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliye mtaka kinyume na nafsi yake, na
hakika yeye ni katika wakweli.
NAMI sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni mno kuamrisha maovu, isipo kuwa ile
ambayo Mola wangu Mlezi aliyo irehemu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Msamehevu na
Mwenye kurehemu.
Basi namna hivi tukampa Yusuf cheo katika nchi; anakaa humo popote anapo penda.
Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupuuzi malipo ya wafanyao mema.
Basi walipo rejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula
zaidi, basi mpeleke nasi ndugu yetu ili tupate kupimiwa; na yakini sisi
tutamlinda.
Je, nikuaminini kwa huyu ila kama nilivyo kuaminini kwa nduguye zamani? Lakini
Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kulinda, naye ndiye Mbora wa kurehemu kuliko wenye
kurehemu wote.
Na walipo fungua mizigo yao wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa. Wakasema: Ewe
baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Wacha tuwaletee
watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na tutaongeza shehena ya ngamia. Na
hicho ni kipimo kidogo.
Akasema: Sitampeleka nanyi mpaka mnipe ahadi kwa Mwenyezi Mungu kwamba lazima
mtamrejeza kwangu, ila ikiwa mmezungukwa. Basi walipo mpa ahadi yao alisema:
Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo.
Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie mlango mmoja, bali ingieni kwa milango mbali
mbali. Wala mimi sikufaeni kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko ila kwa
Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea, na juu yake Yeye wategemee
wanao tegemea.
Na walipo ingia kama alivyo waamrisha baba yao, haikuwafaa kitu kwa Mwenyezi
Mungu, isipo kuwa ni haja tu iliyo kuwa katika nafsi ya Yaa'qub aliitimiza. Na
hakika yeye alikuwa na ilimu kwa sababu tulimfundisha; lakini watu wengi
hawajui.
Na alipo kwisha watengenezea mahitaji yao akakitia kikopo cha kunywea maji
katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mnadi akanadi: Enyi wasafiri! Hapana shaka
nyinyi ni wezi!
Basi akaanza kwenye mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akakitoa katika
mzigo wa nduguye. Hivi ndivyo tulivyo mpangia Yusuf. Hakuweza kumzuia nduguye
kwa sharia ya mfalme isipo kuwa alivyo taka Mwenyezi Mungu. Tunawatukuza kwenye
vyeo tuwatakao; na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi.
Wakasema: Ikiwa huyu ameiba, basi nduguye vile vile aliiba zamani. Lakini Yusuf
aliyaweka siri moyoni mwake wala hakuwaonyesha. Akawaambia: Nyinyi mko katika
hali mbaya zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayo singizia.
Walipo kata tamaa naye wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui
ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kwenu kutokana na Mwenyezi Mungu, na kabla
ya hapo mlimkosa katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi mimi sitotoka nchi hii
mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora
wa mahakimu.
Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Mwanao ameiba. Na sisi hatutoi
ushahidi ila kwa tunayo yajua. Wala sisi hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya
ghaibu.
Akasema: Bali nafsi zenu zimekushawishini kwenye jambo fulani. Subira ni njema!
Asaa Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
Enyi wanangu! Nendeni mkamtafute Yusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraji
ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraji ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa
watu makafiri.
Basi walipo ingia kwa Yusuf walisema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata shida, sisi na
watu wetu. Na tumeleta mali kidogo. Basi tupimie kipimo na fanya kama unatupa
sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka.
Wakasema: Kumbe wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu
yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anaye mcha Mungu na akasubiri,
basi Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa wafanyao mema.
Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka
kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto yangu ya
zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi Mungu amenifanyia
wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya Shet'ani kuchochea
baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole kwa alitakalo. Bila
ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa utawala, na umenifunza tafsiri ya mambo.
Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera.
Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na nichanganyishe na watendao mema.
Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua - mimi na
wanao nifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.
Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipo kuwa wanaume tulio wafunulia wahyi
miongoni mwa watu wa mijini. Je! Hawatembei katika ardhi wakaona jinsi ulivyo
kuwa mwisho wa walio kuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ni bora kwa
wamchao Mungu. Basi hamfahamu?
Hata Mitume walipo kata tamaa na wakaona kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia
nusura yetu, wakaokolewa tuwatakao. Na adhabu yetu haitowawacha kaumu ya
wakosefu.
Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo
zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na
ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.