Kwa hayo Yeye anaizalisha kwa ajili yenu mimea, na mizaituni, na mitende, na
mizabibu, na kila namna ya matunda. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu
wanao fikiri.
Yeye ndiye aliye ifanya bahari ikutumikieni, ili kutokana na humo mpate kula
nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayo yavaa. Na unaona marikebu zikikata maji
humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.
Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Kiyama, na sehemu ya mizigo ya wale
wanao wapoteza bila ya kujua. Angalia, ni maovu mno hayo wanayo yabeba!
Walipanga vitimbi walio kuwa kabla yao, Mwenyezi Mungu akayasukua majengo yao
kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao, na adhabu ikawajia kutoka wasipo
kujua.
Kisha Siku ya Kiyama atawahizi na atasema: Wako wapi hao washirika wangu ambao
kwao mkiwakutisha (Manabii) mashaka? Watasema walio pewa ilimu: Hakika leo ndiyo
hizaya na adhabu itawashukia makafiri,
Ambao Malaika waliwafisha nao wamejidhulumu nafsi zao! Basi watasalimu amri,
waseme: Hatukuwa tukifanya uovu wowote. (Wataambiwa): Kwani! Hakika Mwenyezi
Mungu anajua sana mliyo kuwa mkiyatenda.
Na wataambiwa walio mcha Mungu: Mola wenu Mlezi kateremsha nini? Watasema:
Kheri. Walio fanya wema katika dunia hii watapata wema. Na nyumba ya Akhera ni
bora zaidi, na njema mno nyumba ya wachamngu.
Wanangojea jengine hawa ila Malaika wawafikie, au iwafikie amri ya Mola wako
Mlezi? Kama hivyo walitenda walio kuwa kabla yao. Na Mwenyezi Mungu
hakuwadhulumu, lakini walijidhulumu wenyewe.
Na washirikina wanasema: Mwenyezi Mungu angeli taka tusingeli abudu chochote
badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeli harimisha chochote bila ya
Yeye. Kama hivyo walifanya walio kuwa kabla yao. Basi lipo lolote juu ya Mitume
isipo kuwa kubalighisha kwa uwazi?
Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu,
na muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo alio waongoa Mwenyezi Mungu. Na kati
yao wapo ambao ulio wathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie
ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.
Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa viapo vyao kwamba Mwenyezi Mungu
hatomfufua aliye kufa. Kwani! Ni ahadi iliyo juu yake kikweli; lakini watu wengi
hawajui.
Na wale walio hama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, bila ya
shaka tutawaweka duniani kwa wema; na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi; laiti
kuwa wanajua!
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli wachukulia watu kwa mujibu wa dhulma zao, basi
asingeli mwacha hapa hata mnyama mmoja. Lakini anawaakhirisha mpaka muda ulio
wekwa. Na unapo fika muda wao hawatakawilia hata saa moja wala hawatatangulia.
Na wanampa Mwenyezi Mungu wanavyo vichukia wao, na ndimi zao zinasema uwongo
kwamba wao watapata mema. Hapana shaka hakika wamewekewa Moto, nao wataachwa
humo.
Wallahi! Sisi tulituma Mitume kwa umati zilizo kuwa kabla yako, lakini Shetani
aliwapambia vitendo vyao. Kwa hivyo leo yeye ndiye rafiki yao; nao watapata
adhabu chungu.
Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwa hayo akaihuisha ardhi
baada ya kufa kwake. Kwa hakika katika hayo imo Ishara kwa watu wanao sikia.
Na hakika katika nyama hoa nyinyi mna mazingatio. Tunakunywesheni katika vile
viliomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi mazuri kwa
wanywao.
Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizo
fanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi
mbali mbali; ndani yake kina matibabu kwa wanaadamu. Hakika katika haya ipo
Ishara kwa watu wanao fikiri.
Na Mwenyezi Mungu amekuumbeni; kisha anakufisheni. Na miongoni mwenu wapo wanao
rudishwa kwenye umri mbaya kabisa, hata akawa asijue kitu baada ya ujuzi alio
kuwa nao. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi na Mweza.
Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Na
wale walio fadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ilio wamiliki mikono yao
ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo. Basi je, wanazikataa neema za
Mwenyezi Mungu?
Na Mwenyezi Mungu amekuumbieni wake katika jinsi yenu, na akakujaalieni kutoka
kwa wake zenu wana na wajukuu, na akakuruzukuni vitu vizuri vizuri. Basi je,
wanaamini upotovu na wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa mtumwa aliye milikiwa, asiye weza kitu, na
mwingine tuliye mruzuku riziki njema inayo toka kwetu, naye akawa anatoa katika
riziki hiyo kwa siri na dhaahiri. Je, hao watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi!
Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu, hawezi
chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake. Popote anapo muelekeza haleti kheri. Je!
Huyo anaweza kuwa sawa na yule anaye amrisha uadilifu, naye yuko juu ya Njia
Iliyo Nyooka?
Na siri zote za katika mbingu na ardhi ziko kwa Mwenyezi Mungu. Wala halikuwa
jambo la Saa (ya Kiyama) ila kama kupepesa kwa jicho, au akali ya hivyo. Hakika
Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Je! Hawawaoni ndege walivyo wat'iifu katika anga la mbingu? Hapana mwenye
kuwashika isipo kuwa Mwenyezi Mungu. Hakika katika haya zipo ishara kwa watu
wanao amini.
Na Mwenyezi Mungu amekujaalieni majumba yenu yawe ni maskani yenu, na
amekujaalieni kutokana na ngozi za wanyama nyumba mnazo ziona nyepesi wakati wa
safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na
nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda.