Na ni tangazo kutokana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wote siku ya Hija
Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawana jukumu lolote kwa washirikina.
Basi mkitubu itakuwa kheri kwenu, na mkigeuka basi jueni kuwa nyinyi hamumshindi
Mwenyezi Mungu. Na wabashirie makafiri kuwa watapata adhabu chungu.
Isipo kuwa washirikina ambao mliahidiana nao kisha wasikupunguzieni chochote,
wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu, basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda
wao. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wacha-Mungu.
Na ikisha miezi mitukufu basi wauweni washirikina popote mwakutapo, na washikeni
na wazungukeni, na wavizieni katika kila njia. Lakini wakitubu, wakashika Sala,
na wakatoa Zaka, basi waachilieni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
Mwenye kurehemu.
Na ikiwa mmoja wapo katika washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate
kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahala pake pa amani. Haya ni
kwa kuwa hao ni watu wasiojua kitu.
Itakuwaje iwepo ahadi na washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume
wake, ila wale mlio ahidiana nao kwenye Msikiti Mtakatifu? Basi maadamu
wanakwenda nanyi sawa, nanyi pia nendeni sawa nao. Hakika Mwenyezi Mungu
huwapenda wachamngu
Itakuwaje! Nao wakikushindeni hawatazami kwenu udugu wala ahadi.
Wanakufurahisheni kwa midomo yao tu, na nyoyo zao zinakataa hayo. Na wengi wao
ni wapotovu.
Na wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao, na wakatukana Dini yenu, basi
piganeni na waongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo vya kweli. Huenda (kwa
hayo) wakaacha.
Je, hamtapigana na watu walio vunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumfukuza
Mtume, nao ndio walio kuanzeni mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi
Mungu anastahiki zaidi mumwogope, ikiwa nyinyi ni Waumini.
Je, mlidhani kuwa mtaachwa tu, bila ya Mwenyezi Mungu kuwajuulisha wale walio
pigana Jihadi kati yenu, na wala hawakumfanya mwendani wao isipo kuwa Mwenyezi
Mungu na Mtume wake na Waumini wenziwe? Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za yote
mnayo yatenda.
Haiwi kuwa makafiri ndio waamirishe misikiti ya Mwenyezi Mungu, hali
wanajishuhudishia wenyewe ukafiri. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika, na
katika Moto watadumu.
Hakika wanao amirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale wanao muamini Mwenyezi
Mungu, na Siku ya Mwisho, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka, na wala hawamchi
ila Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa katika waongofu.
Je, mnafanya kuwanywesha maji Mahujaji na kuamirisha Msikiti Mtakatifu ni sawa
na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na akapigana Jihadi
katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi
Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
Wale walio amini, na wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi
Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wana cheo kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi
Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu.
Enyi mlio amini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa vipenzi vyenu ikiwa
wanastahabu ukafiri kuliko Imani. Na katika nyinyi atakaye wafanya hao ndio
vipenzi vyake, basi hao ndio madhaalimu.
Sema: Ikiwa baba zenu, na wenenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na
mali mliyo yachuma, na biashara mnazo ogopa kuharibika, na majumba mnayo
yapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi
katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi
Mungu hawaongoi watu wapotovu.
Hakika Mwenyezi Mungu amekunusuruni katika mapigano mengi, na siku ya Hunayni
ambapo wingi wenu ulikupandisheni kichwa, lakini haukukufaeni kitu. Na ardhi
ikawa dhiki kwenu juu ya upana wake. Kisha mkageuka mkarudi nyuma.
Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya
Waumini. Na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu wale walio
kufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri.
Enyi mlio amini! Hakika washirikina ni najsi, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti
Mtakatifu baada ya mwaka wao huu. Na ikiwa mnakhofia umasikini, basi Mwenyezi
Mungu atakutajirisheni kwa fadhila yake akipenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni
Mwenye kujua Mwenye hikima.
Piganeni na wasio muamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho, wala hawaharimishi
alivyo harimisha Mwenyezi Mungu na Mtume, wala hawashiki Dini ya Haki, miongoni
mwa walio pewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa khiari yao, hali wamet'ii.
Na Mayahudi wanasema: Uzeir ni mwana wa Mungu. Na Wakristo wanasema: Masihi ni
mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya walio
kufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa!
Wamewafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Mwenyezi
Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipo kuwa wamuabudu
Mungu Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayo
mshirikisha nayo.
Enyi mlio amini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu
kwa baat'ili na wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wanao kusanya dhahabu na
fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wabashirie khabari ya
adhabu iliyo chungu.
Siku zitapo tiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya
nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya ndiyo mlio jilimbikia
nafsi zenu, basi onjeni mliyo kuwa mkilimbika.
Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya
Mwenyezi Mungu tangu alipo umba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine
mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na
piganeni na washirikina wote kama wao wnavyo pigana nanyi nyote. Na jueni kuwa
Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.
Bila ya shaka kuakhirisha (miezi) ni kuzidi katika kukufuru; kwa hayo hupotezwa
walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili
wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo
huhalalisha alivyo viharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao
hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Enyi mlio amini! Mna nini mnapo ambiwa: Nendeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu,
mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera?
Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na ya Akhera ni chache.
Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipo
mtoa walio kufuru, naye ni wa pili katika wawili walipo kuwa katika pango, naye
akamwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi.
Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamuunga mkono kwa majeshi msiyo
yaona, na akalifanya neno la walio kufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu
kuwa ndilo juu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima.
Na lau ingeli kuwa ipo faida ya papo kwa papo, na safari yenyewe ni fupi,
wangeli kufuata. Lakini wameona ni mbali na kuna mashaka. Nao wataapa kwa
Mwenyezi Mungu: Tungeli weza bila ya shaka tungeli toka pamoja nanyi.
Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni waongo.
Hawatakuomba ruhusa wale wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wasende
kupigana Jihadi kwa mali yao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua
wachamngu.
Na ingeli kuwa kweli walitaka kutoka bila ya shaka wangeli jiandalia maandalio,
lakini Mwenyezi Mungu kachukia kutoka kwao, na kwa hivyo akawazuia na ikasemwa:
Kaeni pamoja na wanao kaa!
Lau wangeli toka nanyi wasingeli kuzidishieni ila mchafuko, na wange tanga tanga
kati yenu kukutilieni fitna. Na miongoni mwenu wapo wanao wasikiliza. Na
Mwenyezi Mungu anawajua madhaalimu.
Tangu zamani walitaka kukutilieni fitna, na wakakupindulia mambo juu chini,
mpaka ikaja Haki na ikadhihirika amri ya Mwenyezi Mungu, na wao wamechukia.
Na miongoni mwao wapo wanao sema: Niruhusu wala usinitie katika fitina. Kwa
yakini wao hivyo wamekwisha tumbukia katika fitina. Na hakika Jahannamu
imewazunguka.
Sema: Hivyo mnatutazamia litupate lolote isipo kuwa moja katika mema mawili? Na
sisi tunakutazamieni kuwa Mwenyezi Mungu akufikishieni adhabu itokayo kwake, au
kutokana na mikono yetu. Basi ngojeni, nasi tunangoja pamoja nanyi.
Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao ila kwa kuwa walimkataa Mwenyezi Mungu
na Mtume wake, wala hawaji kwenye Sala ila kwa uvivu, wala hawatoi michango ila
nao wamechukia.
Na laiti wao wangeli ridhia kile alicho wapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na
wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila
yake - na pia Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu!
Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa
nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya
Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu ulio faridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na
Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.
Na miongoni mwao wapo wanao muudhi Nabii na kusema: Yeye huyu ni sikio tu. Sema:
Basi ni sikio la kheri kwenu. Anamuamini Mwenyezi Mungu, na ana imani na
Waumini, naye ni rehema kwa wanao amini miongoni mwenu. Na wanao muudhi Mtume wa
Mwenyezi Mungu watapata adhabu chungu.
Wanakuapieni Mwenyezi Mungu ili kukuridhisheni nyinyi, hali ya kuwa wanao
stahiki zaidi kuridhishwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lau kama wao ni
Waumini.
Wanaafiki wanaogopa isije teremshwa Sura itakayo watajia yaliyomo katika nyoyo
zao. Sema: Fanyeni mzaha! Hakika Mwenyezi Mungu atayatoa nje hayo mnayo yaogopa.
Wanaume wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote ni hali moja. Huamrisha maovu na
huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye
pia amewasahau. Hakika wanaafiki ndio wapotofu.
Mwenyezi Mungu amewaahidi wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake na makafiri
Moto wa Jahannamu kudumu humo. Hayo yanawatosha, na Mwenyezi Mungu amewalaani;
nao wana adhabu milele.
Ni kama wale walio kuwa kabla yenu. Walikuwa wana nguvu na mali na watoto zaidi
kuliko nyinyi. Basi walistarehea fungu lao, na nyinyi mnastarehea fungu lenu,
kama walivyo starehe kwa fungu lao wale walio kuwa kabla yenu. Na nyinyi mkazama
katika maovu kama wao walivyo zama. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika
katika dunia na Akhera; na hao ndio walio khasiri.
Je, hazikuwafikia khabari za walio kuwa kabla yao - kaumu ya Nuhu, na A'ad, na
Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa Madyana, na miji iliyo pinduliwa chini
juu? Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa
mwenye kuwadhulumu, walakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi.
Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii
Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi
Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume na Waumini wanawake Bustani zipitazo
mito kati yake, wadumu humo. Na makaazi mema katika Bustani za kudumu, na Radhi
za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao wamekwisha sema neno la ukafiri,
na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakajihimu kufanya ambayo hawakuweza
kuyafikia. Na hawakuchukia ila kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha
kutokana na fadhila zake. Wakitubu itakuwa kheri kwao, na wakigeuka Mwenyezi
Mungu atawaadhibu adhabu chungu duniani na Akhera. Na wala hawana katika ardhi
mlinzi wala wa kuwanusuru.
Na miongoni mwao wapo walio muahidi Mwenyezi Mungu kwa kusema: Akitupa katika
fadhila yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao mema.
Basi akawalipa unaafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapo kutana naye, kwa
sababu ya kuwa walimkhalifu Mwenyezi Mungu katika yale waliyo muahidi, na kwa
sababu ya kusema kwao uwongo.
Wale wanao wabeuwa Waumini wanao toa sadaka nyingi na wasio nacho cha kutoa ila
kadri ya juhudi yao, basi huwakejeli. Mwenyezi Mungu atawakejeli wao! Nao
watapata adhabu chungu!
Waombee msamaha au usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara sabiini, Mwenyezi
Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na
Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotofu.
Walifurahi walio achwa nyuma kwa kule kubakia kwao nyuma na kumuacha Mtume wa
Mwenyezi Mungu. Na walichukia kupigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao, na
wakasema: Msitoke nje katika joto! Sema: Moto wa Jahannamu una joto zaidi, laiti
wangeli fahamu!
Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi kimoja miongoni mwao - na
wakakutaka idhini ya kutoka - sema: Nyinyi hamtatoka pamoja nami kabisa, wala
hamtapigana na adui pamoja nami. Nyinyi mliridhia kukaa nyuma mara ya kwanza,
basi kaeni pamoja na hao watakao bakia nyuma.
Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame kaburini kwake.
Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakafa na hali ni
wapotofu.
Na inapo teremshwa Sura isemayo: Muaminini Mwenyezi Mungu na piganeni Jihadi
pamoja na Mtume wake, wale wenye nguvu miongoni mwao hukutaka ruhusa na husema:
Tuache tuwe pamoja na wanao kaa nyuma!
Lakini Mtume na wale walio amini pamoja naye waliwania Jihadi kwa mali zao na
nafsi zao. Hao ndio watakao pata kheri nyingi, na hao ndio wenye kufanikiwa.
Na walikuja wenye kutoa udhuru katika Mabedui ili wapewe ruhusa, na wakakaa wale
walio mwambia Mwenyezi Mungu na Mtume wake uwongo. Itawafika walio kufuru katika
wao adhabu chungu.
Hapana lawama kwa wanyonge, wagonjwa, na wasio pata cha kutumia, maadamu
wanamsafia niya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hapana njia ya kuwalaumu wanao
fanya wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
Wala wale walio kujia ili uwachukue ukasema: Sina kipando cha kukuchukueni. Tena
wakarudi na macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kukosa cha kutoa.
Ipo njia ya kuwalaumu wale wanao kuomba ruhusa wasende vitani na hali wao ni
matajiri. Wameridhia kuwa pamoja na wanao bakia nyuma. Na Mwenyezi Mungu
amewapiga muhuri juu ya nyoyo zao. Kwa hivyo hawajui.
WATAKUTOLEENI UDHURU mtapo warudia. Sema: Msitoe udhuru; hatukuaminini. Mwenyezi
Mungu amekwisha tueleza khabari zenu. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wataviona
vitendo vyenu. Kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa ya siri na ya dhaahiri; naye
atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
Watakuapieni kwa Mwenyezi Mungu mtakapo rudi kwao ili muwaachilie mbali. Basi
waachilieni mbali. Hakika hao ni najsi, na makaazi yao ni Jahannamu, kuwa ni
malipo kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
Mabedui wamezidi sana katika ukafiri na unaafiki, na wameelekea zaidi kutojua
mipaka ya aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu
ni Mjuzi Mwenye hikima.
Na katika Mabedui hao wapo wanao fikiri kuwa wanayo yatoa ni gharama ya bure, na
wanakungojeleeni mambo yakugeukieni. Mageuko maovu yatakuwa juu yao! Na Mwenyezi
Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
Na katika Mabedui wapo wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na
wanaitakidi kuwa wanayo yatoa ndiyo ya kuwasogeza kwa Mwenyezi Mungu na ya
kuwapatia dua za Mtume. Naam! Hayo ni kweli mambo ya kuwasogeza. Mwenyezi Mungu
atawaingiza katika rehema yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira Mwenye
kurehemu.
Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na walio wafuata
kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na
amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko
kufuzu kukubwa.
Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika wenyeji wa Madina
pia wapo walio bobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu
mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.
Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu.
Asaa Mwenyezi Mungu akapokea toba zao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe
Mwenye kurehemu.
Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee
rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia
Mwenye kujua.
Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali
sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?
Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini wataviona
vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua siri na dhaahiri; naye
atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
Na wapo walio jenga msikiti kwa ajili ya madhara na ukafiri na kuwafarikisha
Waumini, na pa kuvizia kwa walio mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake hapo
kabla. Na bila ya shaka wataapa kwamba: Hatukukusudia ila wema tu. Na Mwenyezi
Mungu anashuhudia kuwa wao ni waongo.
Usisimame kwenye msikiti huo kabisa. Msikiti ulio jengwa juu ya msingi wa
uchamngu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame ndani yake. Humo
wamo watu wanao penda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanao jitakasa.
Je! Mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu ya kumcha Mwenyezi Mungu na radhi
zake ni bora au mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu ya ukingo wa shimo linalo
burugunyika, na likaburugunyika naye katika Moto wa Jahannamu? Na Mwenyezi Mungu
hawaongoi watu madhaalimu.
Na jengo lao hilo walilo lijenga litakuwa sababu ya kutia wasiwasi nyoyoni mwao
mpaka nyoyo zao hizo zikatike vipande vipande. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua
Mwenye hikima.
Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao
watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu - wanauwa na wanauwawa.
Hii ni ahadi aliyo jilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur'ani. Na
nani atimizae ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo
fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa,
Wala haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila kwa sababu wa ahadi aliyo
fanya naye. Lakini ilipo mbainikia kwamba yeye ni adui ya Mwenyezi Mungu,
alijiepusha naye. Hakika Ibrahim alikuwa mwingi wa kuomba, mnyenyekevu,
mvumilivu.
Na haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwahisabu watu kuwa wamepotea baada ya kwisha
waongoza mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye
kujua kila kitu.
Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari walio mfuata
katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi
akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.